Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wenye viwanda na waajili wote nchini wametakiwa kufungua milingo ya kuwapatia vijana mafunzo kwa vitendo kwenye vyuo vya VETA.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Carolyne Nombo,wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wamiliki wa viwanda, waajiri na wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika ukumbi wa Mlimani City.

Amesema kukutana kwao ni sehemu muhimu ya kutafuta suluhisho la pamoja kuhusu fursa za ajira zilizopo, katika sekta mbalimbali nchini pamoja na ukuaji wa viwanda na maendeleo ya Taifa letu kiuchumi.
‘’Mkutano huu utakuwa mahususi ni kuhakikisha tunazalisha nguvu kazi yenye ujuzi, umahiri na ubunifu unao kidhi mahitaji ya sasa na ya baadae ya soko la ajira na maendeleo ya viwanda nchini kwa kuzingatia ushindani uliopo ‘’amesema.
Profesa Carolyne amesema Serikali imelenga kuimarisha ubora wa elimu na mafunzo nchini hususan kwenye eneo hili la ufundi stadi ili kuongeza ushirikiano kati ya taasisi za mafunzo na sekta binafsi kwa kuhakikisha wananchi wanapata fursa za kujifunza na kujiendeleza.

‘’Ni ukweli usiopingika kwamba Viwanda ndivyo vinavyoendana kwa kasi na mabadiliko ya teknolojia katika nyanja zote hivyo, ni fursa muhimu kwa vijana wetu kupata mafunzo ya vitendo sehemu za kazi ili kupambana na soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Ushiriki wa wanafunzi kwenye mafunzo ya vitendo katika mazingira halisi ya kazi inawawezesha kuelewa teknolojia mpya, kujenga uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi na kuwa wabunifu na washindani katika soko la ajira la sasa na la baadae.
Mkurugenzi mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore, amesema kwa sasa kuna VETA inasimamia vyuo 80 vinavyotoa mafunzo. kwa mwaka kupitia kozi za muda mrefu na mfupi.

Amesema mkutano wa wadau hao ni muhimu kwao kwa kuhakikisha wanatoa mafunzo yenye ubora kwani tunahitaji wafanyakazi wao waweze kuja kwetu kuongezewa ujuzi ili waweze kuwa bora kwenye ufanisi wa kazi zao.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya VET, Clotilda Ndezi amesema bodi imeendelea kutoa msukumo mkubwa katika kuhakikisha mafunzo ya ufundi stadi nchini yanakuwa ya vitendo zaidi na yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira.
‘’Tunatambua kuwa ili mwanafunzi awe na umahiri wa kweli, anapaswa kujifunza na kujaribu kwa vitendo kwa kile anachofundishwa darasani.
Ndiyo maana ,bodi imekuwa ikisisitiza katika sera zake na miongozo kuwa mitihani na tathmini za wanafunzi zijikite zaidi kwenye vitendo kuliko nadharia.’’amesema
Aidha, tunatambua kuwa mafanikio ya mkakati huu hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa karibu na sekta ya viwanda na waajiri wa sekta mbalimbali.

Hivyo, Bodi ya VET inawaomba na wenye viwanda na waajiri kutoa fursa pana za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa ufundi stadi (field attachment na apprenticeship), ili kuongeza umahiri wao katika ajira.
Amesema lengo la bodi ni kuhakikisha tunazalisha wahitimu wanaoweza kufanya kazi kwa ufanisi pindi wanapoingia kazini.
