Mgombea ubunge wa Jimbo la Tanganyika, mkoani Katavi, Selemani Moshi Kakoso, amesema kuwa Wilaya ya Tanganyika imenufaika kwa kiasi kikubwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita chini ya uongozi wa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ameyasema hayo Oktoba 18, 2025, katika muendelezo wa kampeni za mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema kuwa, kupitia fedha za maendeleo, Wilaya ya Tanganyika imenufaika na zaidi ya shilingi bilioni 558 ambazo zimewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara, maji, umeme na bandari.
Aidha, amebainisha kuwa serikali imetoa shilingi bilioni 57 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kuu kutoka Mpanda Mjini kuelekea Kigoma, ambapo kilometa saba zimekamilika na kilometa 25 zinaendelea kukamilishwa kati ya kilometa 37 zilizopangwa kujengwa.
Ameeleza kuwa dhamira yake ni kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Kigoma kupitia ujenzi wa barabara ya kimkakati ya kiuchumi kutoka eneo la Maziwa Makuu kuelekea Karema.
Pia, amebainisha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 48 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Karema, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri wa majini. Amesema kuwa kwa sasa kuna ujenzi wa meli nne zinazounganisha Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kakoso amesema kuwa sekta ya maji nayo imeboreshwa, ambapo awali Wilaya ya Tanganyika ilikuwa na upatikanaji wa maji safi kwa asilimia 36, lakini kwa sasa upatikanaji huo umefikia asilimia 80.
Aidha, amebainisha kuwa katika sekta ya umeme, vijiji vyote 55 vya Wilaya ya Tanganyika sasa vimeunganishwa na umeme, ikiwemo umeme wa gridi ya taifa.
Amesema kuwa sekta ya kilimo pia imenufaika kupitia ruzuku ya pembejeo, hatua iliyowasaidia wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Kakoso amebainisha kuwa sekta ya afya nayo imepiga hatua, ambapo vituo vya afya vimeongezeka kutoka vitatu hadi kufikia kumi, japokuwa bado kuna changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya na huduma za lishe katika vituo hivyo.
Aidha, amebainisha kuwa bado kuna haja ya kukamilisha barabara ya kutoka Mpanda kuelekea Karema na Kigoma ili kuunganisha Bandari ya Karema na Bandari ya Dar es Salaam kwa ufanisi zaidi.




