Na Mwandishi Maalum
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameungana na Ubalozi wa Jamhuri ya Uturuki nchini katika hafla ya kuadhimisha Miaka 102 ya Kuundwa kwa Jamhuri ya Uturuki iliyofanyika Oktoba 17,2025 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Waziri Kombo aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Uturuki Mheshimiwa Recep Tayyip Erdoğan na wananchi wa Utüruki, akiwapongeza kwa mafanikio makubwa katika maendeleo, amani na umoja wa kitaifa.

Mhe. Kombo alisisitiza dhamira ya Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano na Uturuki hasa katika maeneo ya diplomasia, biashara, uwekezaji, elimu, afya, usafiri, ulinzi, utamaduni na utalii.
Ameishukuru Jamhuri ya Uturuki kwa kuimarisha ushirikiano na Tanzania akitaja ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa (SGR) unaotekelezwa na kampuni ya Kituruki, Yapi Merkezi; ongezeko la biashara kati ya nchi hizo mbili na fursa za ufadhili wa masomo kwa Watanzania nchini Uturuki.
Aidha, Mhe. Kombo amelishukuru Shirika la Maendeleo la Uturuki (TIKA) kwa kuchangia miradi mbalimbali ya Maendeleo ikiwemo ya afya, michezo na mazingira nchini, kwani imechangia kuleta maendeleo ya jamii nchini.

Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Mhe. Bekir Gezer aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na urafiki wake, akisisitiza utayari wa Uturuki kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wa pande zote.
Mhe. Gezer pia aliwasilisha salaam zake za kuitakia heri na amani Tanzania, katika uchaguzi wake mkuu utakaofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali, wanadiplomasia na wanajamii wa Uturuki wanaoishi nchini.



