Na Mwandishi Wetu,Nairobi
Shirika la kimataifa la Article 19, Afrika ya Mashariki, limeahidi kushirikiana na chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari Tanzania(JOWUTA) kusaidia kuwajengea uwezo wanahabari katika masuala ya utetezi wa sheria za habari, haki za wanahabari na ukatili kwa wanahabari wanawake.
Makubaliano ya ushirikiano huo, yamefanyika jijini Nairobi, baina ya JOWUTA na Article 19, mara baada ya mkutano wa taasisi za vyombo vya habari katika nchi za Afrika ya Mashariki,kujadili masuala ya uhuru wa vyombo vya habari, ushirikiano na utetezi wa wanahabari.

Naibu Mkurugenzi wa Article 19, Patrick Mutahi akizungumza na Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma alisema taasisi hiyo inatambua changamato za sekta ya habari katika nchi za Afrika ya Mashariki ikiwepo Tanzania na itafanyakazi na JOWUTA.
Mutahi alisema, kutokana na changamoto hizo, Article 19 kwa kushirikiana na wahisani wake kadhaa ikiwepo Jumuiya ya Madola( commonwealth) itakuwa na mradi wa kusaidia sekta ya habari katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda.
“Tumepata faraja kukutana katika mkutano huu kujadili changamoto za masuala ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari katika nchi za Afrika ya Mashariki na kuona ni jinsi gani tunaweza kushirikiana kukabiliana na changamoto hizi”alisema
Mutahi alisema, Article 19, itatoa usaidizi kwa JOWUTA katika uketelezaji wa miradi ya kusaidia wanahabari ili kuhakikisha wanahabari wanafanyakazi katika mazingira ya uhuru na kutokuwa na changamoto nyingi.
Juma akizungumza na Mkurugenzi huyo, alimuhakikishia kuwa JOWUTA ni chombo cha wanataaluma wa habari, ambacho kinauwezo wa kutekeleza miradi ya ushirikiano na Article 19 na taasisi nyingine.

Alisema JOWUTA ambayo inawanachama zaidi ya 400 katika mikoa yote nchini Tanzania,inahitaji ushirikiano kuwasaidia wanahabari kufanyakazi katika mazingira bora, wanahabari kuweza kuwa na uwezo wa kiuchumi lakini pia kuweza kushiriki katika majadiliano na waajiri katika kupata hali bora kazini.
“Tunaimani ushirikiano baina ya Article 19 na JOWUTA utakuwa na manufaa makubwa kwa wanahabari nchini Tanzania,ikiwepo pia kubadilishana uzoefu na na wanahabari katika nchi nyingine ili kuhakikisha wanafanyakazi katika mazingira mazuri”alisema
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa programu na mafunzo wa chama cha waandishi wa kujitegemea nchini Kenya(KCA),Willian Oloo-Janak alisema changamoto za sekta ya habari katika nchi za Afrika ya Mashariki kwa kiasi kikubwa zinafanana.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hizo ni muhimu kushirikiana ikiwepo kufanyakazi pamoja na taasisi za kikanda ikiwepo Jumuiya ya Afrika ya Mashariki(EAC) na nyingine kadhaa.

Katika mkutano huo,vyama vya wanahabari Afrika ya Mashariki, vilikubaliana kufanyakazi kwa ushirikiano, kubadilishana uzoefu ,kuwa na mkakati wa pamoja kufanya utetezi wa kupata sheria nzuri za habari,lakini kuwa na sera rafiki ikiwepo ya hali bora za wanahabari na masuala ya kupinga ukatili dhidi ya wanahabari wanawake .
Vyama vingine vilivyoshiriki mkutano huo ni Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA) ,chama cha waandishi wa habari nchini Rwanda, chama cha waandishi wa habari wa kujitegemea Kenya, chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari Kenya, Taasisi ya wanahabari wa mashinani Kenya, Wanahabari Uganda na Mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu Uganda.
