Baada ya mikutano mikubwa iliyofanyika katika maeneo ya Mpanda, Kibaoni na Namanyere (Nkasi), leo ni zamu ya Sumbawanga mjini, ambapo Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufanya mkutano mkubwa wa kampeni.

Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wamekuwa katika shamrashamra za maandalizi ya kumpokea kiongozi huyo, ambapo idadi kubwa ya wananchi inatarajiwa kufurika katika viwanja vya mkutano huo, kama ishara ya imani na upendo wao kwa kazi kubwa alizozifanya katika kipindi chake cha uongozi.

Kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, wananchi wa Rukwa wamekuwa wakionesha hamasa kubwa katika kuunga mkono sera na ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, hasa katika maeneo ya miundombinu, elimu, afya, kilimo na nishati vijijini, ambavyo vimekuwa kipaumbele katika serikali ya awamu ya sita.

Kauli mbiu inayosikika katika mikutano mbalimbali ni “Tunaendelea na Mama hadi 2030”, ikimaanisha dhamira ya wananchi kuendeleza maendeleo endelevu chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kadri kampeni zinavyoelekea ukingoni, wananchi wote wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Oktoba 29, na baada ya kupiga kura kurudi majumbani kwa amani wakisubiri matokeo, ili kulinda utulivu, umoja na amani ya taifa.