Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga amezikwa nyumbani kwao huko Kang’o ka Jaramogi eneo la Bondo, Kaunti ya Siaya.

Mwili wa Raila ulipigiwa mizinga 17 ya risasi kumpatia heshima kulingana na wadhfa aliokuwa nao katika sherehe ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) .

Heshima hizo kamili za kijeshi ziliendeshwa kuambatana na tangazo la rais lililotolewa na Rais William Ruto mara baada ya kifo cha Raila kutangazwa.

Maagizo hayo yaliamuru kwamba kiongozi huyo mkongwe wa upinzani na kiongozi wa serikali afanyiwe mazishi rasmi ya heshima kamili ya kitaifa na kijeshi, kulingana na mchango wake kwa nchi.

Katika hafla hiyo, jeneza lililokuwa limefunikwa kwa bendera ya Kenya liliwekwa chini ya ulinzi mkali wa kijeshi huku wanafamilia na viongozi wa karibu wakikusanyika katika eneo la Kang’o ka Jaramogi, mahali pa kupumzika pa mwisho pa babake Raila, Makamu wa kwanza wa Rais wa Kenya Jaramogi Oginga Odinga.

Saa 4.53 kamili asubuhi, kitengo cha mizinga ya KDF kilifyatua risasi 17 hewani, kila mlipuko ukivuma katika uwanja wa Bondo, kuashiria heshima kubwa ya taifa kwa huduma ya maisha ya Raila kwa demokrasia, haki na uhuru.