Mkazi wa Mtaa wa Msufini Kata ya Kibaha Mjini mkoani Pwani, Asha Madamde, maarufu Bibi Hatibu mwenye miaka 120 ,amesisitiza kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, huku akimuombea dua mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Rais Samia Suluhu Hassan.
Licha ya umri wake mkubwa wa miaka 120, Bibi Hatibu amesema kuwa afya yake na nguvu za Mungu zimemuwezesha kuendelea kushiriki katika shughuli muhimu za kijamii, ikiwemo kutimiza haki yake ya msingi ya kupiga kura.
Bibi huyo amemuombea dua Rais Samia na kuitakia mafanikio makubwa CCM wakati wa kampeni ya nyumba kwa nyumba inayoongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Kibaha Mjini, Elina Mgonja, pamoja na kamati ya utekelezaji ya UWT.
Bibi Hatibu ameeleza, amani ni tunu ya Tanzania, na uchaguzi ni suala nyeti kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Elina Mgonja, Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini, amemshukuru Bibi Hatibu kwa dua yake kwa mgombea urais Samia na kusema kwamba anastahili ushindi wa kishindo kutokana na kazi kubwa aliyofanikisha katika kipindi chake cha uongozi.
Kampeni hizo zinaendelea lengo kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana na kueleza mipango ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025–2030.
