Mgombea Ubunge wa Jimbo la Rufiji kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mohammed Nchebgerwa, amesema kuwa kizazi cha leo kinakwenda kushuhudia historia mpya ya taifa, akibainisha kuwa taifa limewahi kushuhudia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa Rais wa Tanganyika, na sasa kizazi hiki kinashuhudia kiongozi mpya anayependwa kuchaguliwa kupitia sanduku la kura, mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ameyasema hayo Oktoba 20, 2025, katika muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Dkt. Samia, taifa limeshuhudia mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, miundombinu na kilimo. Amesema kuwa kabla ya kipindi hicho kulikuwa na hali duni hasa katika sekta ya afya, ambapo kulikuwepo vituo vitatu pekee, lakini sasa vimeongezeka huku vituo vingine vinne vikiendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali.
Ameeleza kuwa sekta ya miundombinu imepiga hatua kubwa, ambapo barabara ambazo awali hazikuwepo sasa zimejengwa kwa urefu wa takribani kilomita ishirini, pamoja na ujenzi wa madaraja yenye thamani ya shilingi bilioni ishirini na saba, ikiwemo daraja lililoathirika na mafuriko makubwa ya mvua linalojengwa kwa gharama ya shilingi milioni kumi na saba.
Katika sekta ya elimu, amesema kuwa Dkt. Samia amewezesha ujenzi wa shule nyingi ambapo awali kulikuwepo shule nne za sekondari, na sasa zimeongezeka hadi ishirini na nne, huku shule za msingi zikiongezeka kutoka kumi na tisa hadi sitini na tatu.
Aidha, amebainisha kuwa katika sekta ya afya, Serikali ya Awamu ya Sita imejenga zahanati arobaini na mbili na kufanya ukarabati wa hospitali kongwe zikiwemo zilizojengwa tangu enzi za Baba wa Taifa. Amesema hospitali mpya 129 zimejengwa na 119 kukarabatiwa, huku hospitali 48 kongwe zikifanyiwa ukarabati mkubwa.
Amesema kuwa huduma za hewa tiba ambazo awali zilipatikana katika hospitali za mikoa na rufaa, sasa zimeanza kupatikana hadi katika ngazi za halmashauri, ikiwemo Wilaya ya Mafia — hatua inayosaidia kuokoa maisha ya wagonjwa mahututi waliokuwa wanakosa huduma hizo.
Amesema kuwa Dkt. Samia ni mwanamapinduzi wa karne hii, ambaye ameleta mapinduzi ya kiuchumi kwa kusogeza huduma karibu na wananchi, kuvutia wawekezaji na kufanikisha ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, likitimiza ndoto za Baba wa Taifa.







