Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Kigoma

Kampeni zinaelekea ukingoni. Tumeshuhudia mikikimikiki ya vyama vinavyoshiriki. Tumeshuhudia mikutano ya hadhara. Idadi ya watu wanaoshiriki kwenye mikutano inatosha kukwambia kuwa Watanzania wana matumaini na mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan.

Mwaka huu tumeshuhudia Ilani ya CCM katika mfumo tofauti.

Sitanii, nitaorodhesha ahadi chache kati ya nyingi alizotoa mgombea urais wa CCM, Dk. Samia, ila kabla sijafanya hivyo, nieleze jambo lililonivutia katika Ilani ya CCM mwaka huu.

Tumezoea kuona Ilani kuu ya kitaifa. Ilani inayozungumzia masuala mbalimbali katika ngazi ya kitaifa. Zamu hii Ilani ya CCM iko tofauti.

Ilani hii imefanya uchambuzi wa hadi ngazi ya kata. Kila kata ina kijitabu chake kinachoeleza watafanyiwa nini. Haya ni mapinduzi makubwa.

Ilani ni mkataba kati ya viongozi na wananchi. Suala linalokuwa halipo kwenye Ilani ya uchaguzi, linaweza kutekelezeka ila kwa hisani.

Zamu hii CCM imeamua kuchambua ahadi zinazopatikana kwenye Ilani kwa lugha nyepesi ambayo kila awaye anaielewa. Kichwa cha makala hii kimebebwa na elimu.

Katika mikoa mbalimbali aliyokwenda Rais Samia, ambaye ni mgombea wa CCM, ameeleza kwa kina suala la elimu.

Mgombea huyu wa CCM amesema bayana kuwa serikali yake ikichaguliwa, watoto wote wa Watanzania watapatiwa mikopo ya elimu ya juu bila kujali uwezo wa familia (means testing).

Sera hii inatuondoa Watanzania katika mkwamo. Watoto wengi kutoka familia maskini wamekosa mkopo kwa sababu ya hivi vigezo vya uwezo wa familia. Kigezo cha usawa kilipotea katika mfumo wa elimu.

Sitanii, wapo watoto wanaokosa mkopo kwa maelezo kuwa eti baba yake alikuwa Ofisa Mwandamizi, kumbe hata alipostaafu, akaishiwa kabisa.

Mtoto anaadhibiwa kwa baba au mama yake kupata wadhifa, iwe serikalini au kwenye sekta binafsi. Kumbe zipo nyakati wazazi walikuwa na wadhifa mkubwa, ila mapato kidogo.

Hii imehangaisha familia nyingi kwa kiwango cha kuacha kilio. Asante Rais Samia kwa kulipatia ufumbuzi hili.

Ikiwa CCM itachaguliwa na kupewa ridhaa ya kuongoza kati ya sasa mwaka 2025 na 2030, kupitia Ilani yake ya uchaguzi, imelenga kukuza ukuaji wa uchumi kwa kiwango cha angalau asilimia saba (7%) ya ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) mwaka baada ya mwaka.

Analenga kuongeza ukuaji wa kilimo kwa 10% ifikapo 2030, kwa njia ya kuongeza kilimo cha umwagiliaji, pembejeo nafuu, na teknolojia, hasa baada ya mavuno.

Ilani ya CCM inalenga kuzalisha ajira nyingi kupitia ukuaji wa viwanda, huduma, kilimo na sekta nyingine. Eneo la viwanda wanalenga kuimarisha sekta ya viwanda na kuongeza thamani ya malighafi za ndani (value addition) — mfano: kuanzisha na kuimarisha viwanda vya malighafi za ndani kama mbolea, chakula, dawa na nguo.

CCM imejipanga kuboresha utoaji wa huduma za kijamii: elimu, afya, maji safi na taka. Katika elimu wanapanga kuhakikisha elimu ya msingi kwa kila mtoto ni hadi sekondari bila ada, uboreshaji wa vituo vya afya, barabara na miundombinu.

Katika kudhibiti deni la taifa, CCM inalenga kuhakikisha mikopo ya umma inatumika kwa miradi ya maendeleo yenye athari kwa kijamii.

Wanalenga kuimarisha miundombinu kama barabara, reli (mfano SGR), bandari, n.k., ili kusaidia usafirishaji, biashara na muunganiko wa kiuchumi.

Mikoa ya Kusini itajengewa reli mpya ya SGR yenye urefu wa kilomita 1,000. Inajengwa reli ya SGR kutoka Tanga, Kilimanjaro – Arusha hadi Musoma (Mara).

Wamejipanga kuendeleza teknolojia, uchumi wa dijitali, na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika uchumi wa kikanda na kimataifa. CCM imeahidi pia kuwa itahakikisha amani, usalama, umoja wa kitaifa, utamaduni na michezo  vinakuwa sehemu ya maendeleo ya kijamii pamoja na kiuchumi.

Kwa vyovyote iwavyo, kuna kila dalili kuwa Tanzania inakwenda kuandika historia ya kupata Rais wa kwanza mwanamke, ambaye ameahidi ndani ya siku 100 kuhakikisha analeta maridhiano miongoni mwa Watanzania na kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya. Mambo ni mengi, ila dalili ya mvua ni mawingu. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827