Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WAZAZI na walezi nchini wametakiwa kutowanyima watoto wao fursa ya kuendelea na elimu nje ya mfumo rasmi pale wanapofeli au kupata ufaulu mdogo katika mitihani yao, kwani huo si mwisho wa safari ya elimu kwa mtoto.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Meneja wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Kampasi ya Dar es Salaam, Dkt. Joshua Mushi, wakati wa mahafali ya 19 ya wanafunzi wa kidato cha nne wa Shule Huria ya Ukonga Skillfull.

Dkt. Mushi alisema mwanafunzi anayefeli au kupata ufaulu wa chini anaweza bado kufikia malengo yake ya kielimu kupitia mfumo wa elimu usio rasmi, ambao hutoa nafasi ya kupata maarifa na ujuzi vitakavyomwezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
“Anayepata ufaulu mdogo au anayefeli kabisa atambue kuwa huo si mwisho wa safari yake ya kielimu. Ipo fursa nje ya mfumo rasmi wa elimu. Shule Huria kama Ukonga Skillfull ni mfano mzuri ambao mwanafunzi anaweza kupata elimu na kuendeleza malengo yake,” alisema Dkt. Mushi.
Amefafanua kuwa wanafunzi wanaosoma katika shule huria na wale wa mfumo rasmi wote wanaweza kukutana vyuoni, ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) au vyuo vingine duniani, kwa kuwa wote watakuwa na sifa zinazofanana.

Aidha, Dkt. Mushi aliwataka wadau wanaotoa elimu nje ya mfumo rasmi kuhakikisha vituo vyao vinasajiliwa na kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali, akibainisha kuwa Ukonga Skillfull ni miongoni mwa shule chache huria nchini zilizosajiliwa rasmi na zinazotoa elimu kwa mujibu wa sheria.
“Niwapongeze Ukonga Skillfull kwani ni moja ya shule chache huria nchini zinazofanya vizuri. Ina waajiriwa zaidi ya 70 na matawi matatu yanayofanya kazi kikamilifu. Wadau wengine wanaotoa elimu nje ya mfumo rasmi waje kujifunza hapa,” alisisitiza Dk. Mushi.
Aliongeza kuwa TEWW inaendelea kuratibu na kufuatilia utoaji wa elimu nje ya mfumo rasmi nchini, ikiwemo kufanya tafiti na kutoa mapendekezo ya maboresho ya mfumo huo ili uweze kuwafikia Watanzania wengi zaidi.
Kwa upande wake, Muasisi na Mwanzilishi wa Shule Huria ya Ukonga Skillfull, Diodorus Tabaro, alisema jumla ya wanafunzi 206 kutoka matawi matatu ya shule hiyo wanatarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwezi Novemba mwaka huu.

Tabaro alibainisha kuwa mahafali hayo yalihusisha wanafunzi wa kidato cha nne na wale wanaorudia mtihani kutoka matawi ya Gongo la Mboto, Mbezi Luis na Tegeta, ambapo wote wameandaliwa vyema kwa ajili ya mtihani wa taifa.
“Wahitimu hawa tumeandaa vizuri na tunaamini watapata matokeo mazuri. Falsafa yetu ni kutoa elimu yenye kuleta mabadiliko chanya ya kitabia, kwa sababu tunaamini mafanikio ya mwanafunzi yanaanza na tabia njema,” alisema Tabaro.

