Tume ya Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini imekutana na wadau wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji, wanunuzi na wathaminishaji wa madini, kwa lengo la kupanga bei elekezi za madini ya vito, hatua inayolenga kuimarisha uwiano wa faida, kuongeza mapato ya Serikali na kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumza jijini Dodoma leo Oktoba 24, 2025, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini CPA. Venance Kasiki, amesema kikao hicho kimefanyika kwa ajili ya kufanya tathmini na kuweka bei mpya zitakazotumika kwa kipindi cha miezi mitatu, kwa kuzingatia mwenendo wa soko la dunia na gharama halisi za uzalishaji.

“Kupitia bei elekezi tunahakikisha wachimbaji, wanunuzi na Serikali wote wananufaika kwa uwiano. Serikali itapata mapato yake kupitia Mrabaha na Ada ya Ukaguzi, huku biashara ikiendelea kwa uwazi na ushindani wa haki,” amesema Kasiki.

Amesema hatua hiyo itaimarisha uthabiti wa soko, kuzuia upotevu wa mapato, na kujenga uaminifu kati ya wadau wa sekta ya madini ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa.

“Bei hizi zitakuwa wazi na zitapatikana kupitia tovuti ya Tume ya Madini na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa. Tunataka wadau wote wapate taarifa sahihi ili kuondoa mianya ya udanganyifu na kuongeza ufanisi wa biashara ya vito nchini,” amesisitiza.

Aidha, Kasiki amesema Tume itaendelea kukutana na wadau kila robo mwaka kwa ajili ya kufanya mapitio ya bei, kujadili changamoto kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika uthaminishaji wa madini duniani.

Kwa upande wake, Kulwa Mkalimoto, Katibu wa Vito kutoka Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), ameeleza kuwa bei elekezi zilizopitishwa ni rafiki kwa wadau wote na zitasaidia kuleta uwiano wa faida katika mnyororo mzima wa sekta ya madini.

“Kikao kimeenda vizuri, bei zilizowekwa ni rafiki na zinaleta usawa. Wachimbaji watanufaika, wanunuzi watanufaika, na Serikali itakusanya mapato yake kupitia Mrabaha, Ada ya Ukaguzi, HIV Response Levy na Ushuru wa Huduma unaokusanywa na halmashauri,” amesema Mkalimoto.

Kikao hicho pia kimeshirikisha vyama mbalimbali vya wadau wa sekta ya madini ikiwemo Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA), FEMATA, Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA), na Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMMATA).