Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeidhinisha Shilingi Billioni 426.5 awamu ya kwanza kwa ajili ya wanafunzi wanufaika 135,240 ili kugharamia masomo yao.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, Oktoba 24, 2025, alipokuwa akiongea na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Ofisi ya HESLB Jijini Arusha. “Tunapenda kuutarifu Umma wa Tanzania kuwa HESLB imeidhinisha Bilioni 426.5 kwa ajili ya wanafunzi 135,240 kwa awamu ya kwanza,” amesema Dkt. Kiwia.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiwia amesisitiza kuwa katika fedha hizo, Shilingi Bilioni 152 zimegharamia wanafunzi 40,952 wa Shahada ya awali na 5,342 wa Stashahada. Aidha, waombaji mikopo wa Samia Skolashipu wapatao 615 wameidhinishiwa Shilingi Bilioni 3.3 huku Shilingi Bilioni 271.2 zikiidhinishwa kwa ajili ya wanafunzi 88,331 wanaendelea na masomo yao katika vyuo mbalimbali hapa nchini.
Ikumbukwe kuwa Bodi ya Mikopo kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2025/2026, imeidhinishiwa Shilingi Bilioni 916.7 ambazo zinategemewa kuwanufaisha wanafunzi 252,773 ili kutimiza ndoto zao za kupata elimu ya kati na ya juu.






