Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

WATOTO yatima wanaolelewa katika Kituo cha Mafanikio Day Care kilichoko Mjini Tabora wamefanya dua maalumu ya kumwombea Dk Samia Suluhu Hassan ili apate ushindi wa kishindo mwaka huu ili aendelea kusaidia wananchi.

Wakisoma dua hiyo kwa niaba ya watoto wenzao zaidi ya 100 wasiojiweza wanaolelewa na kusomeshwa na Kituo hicho, Hanifa Abdallah (4) na Munir Mussa (5) wamemwomba Mwenyezi Mungu amjalie afya njema na kumfanyia wepesi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Wamesema kuwa Mwenyezi Mungu anapendezwa na wale wanaojitoa usiku na mchana kusaidia wananchi wasio na uwezo na kuwatumikia kwa moyo wa upendo pasipo kinyongo ndani ya mioyo yao.

‘Ee Mwenyezi Mungu tunakuomba umjalie afya njema mama yetu Dk Samia Suluhu Hassan, mwepushie balaa yeye na wasaidizi wake na wale wote wenye dhamira ya kuleta machafuko katika kipindi hiki uwashughulikie’, wameomba.

Aidha wamemwomba Mwenyezi Mungu amfanyie wepesi katika uchaguzi Mkuu wa mwaka ili apate kura za kutosha na kuendelea kuwatumikia watanzania ikiwemo kudumisha amani na utulivu hapa nchini.

Pia wamemwomba Mungu aepushie mbali aina zote za vurugu, uchochezi na uvunjifu wa amani katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani Oktoba 29 mwaka huu.

Wamesisitiza kuwa Rais Samia ni Kiongozi mpenda amani, ndiyo maana wakati anaingia madarakani alikaa meza moja na Viongozi wa upinzani na kuanzisha mazungumzo ya maridhiano, huu ni uungwana mkubwa.

Mtoto Zena Juma (5) akizungumza baada ya dua hiyo, ameeleza kuwa nchi ikiingia kwenye machafuko, watoto ndio watakaoathirika zaidi kwa kuwa watakosa msaada wa chakula na elimu, hivyo kupoteza maisha.

Ameomba Mwenyezi Mungu amjalie Dk Samia ushindi ili aendelee kuongoza nchi na kusaidia wananchi wenye mahitaji mbalimbali ikiwemo watoto yatima wanaolelewa katika Kituo hicho.

‘Tunamshukuru sana mama, kwa kutuletea msaada hapa shuleni, tunaomba aendelee kutusaidia, ndiyo maana leo tumefanya dua ili kumwombea kheri kwa Mwenyezi Mungu, amlinde na kumfanyia wepesi katika uchaguzi huu’, alisema.