Mgombea Mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema Watanzania wameridhishwa na utendaji kazi wa mgombea urais wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan.
Dk Nchimbi ametoa kauli hiyo alipopewa nafasi ya kusalimia maelfu ya wananchi wakati wa mikutano wa kuhitimisha kampeni za chama hicho kwenye uwanja wa CCM Kirumba,jijini Mwanza leo Oktoba 28,2025.
“Nakushukuru sana mgombea urais wa Tanzania kupitia chama chetu kwa imani yako kubwa kwangu kwa kunipendekeza kuwa msaidizi wako mkuu.
“Miaka minne iliyopita uliniteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misiri, baadae ukanipendekeza kupitia vikao vya Halmshauri Kuu ya CCM Taifa kuwa Katibu Mkuu wa CCM na sasa umeniamini katika nafasi ya mgombea mwenza.
“Katika kipindi cha miaka minne umeonesha imani yako kwangu kwa kunipa nafasi muhimu ndani ya Taifa letu na ndani ya CCM
“Nakuhakikishia imani uliyoonesha, namna pekee ninayoweza kuilipa ni kukusaidia kwa nguvu, akili, maarifa na uaminifu ili ndoto na maono yako na utekelezaji wa ilani yetu ya CCM (2025/30) ufanyike kwa mafanikio makubwa katika miaka mitano ijayo “amesema.

Amesema katika mikoa mbalimbali aliyopita wakati wa mikutano ya kampeni Watanzania wameonyesha imani kubwa kwa Rais Samia kutokana na kazi nzuri aliyofanya.
“Watanzania katika sehemu zote tulizopita wameridhika na utekelezaji wako wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/25 kwa kishindo, wametutuma tukueleze kuwa kesho watakupa kura nyingi za ushindi wa kishindo,
“Hili linatokana na utendaji kazi wako katika Serikali ya awamu ya sita unayoiongoza inayotakana na Chama Cha Mapinduzi (CCM)..”
Mwisho


