Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maendeleo Jijini Dodoma kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji Tanzania (TACTIC) kuhakikisha wanakamilisha kazi kwa wakati, ili kufikia malengo ya Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo, Mhe. Senyamule amesema Serikali inawekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, madaraja na masoko, hivyo ucheleweshaji wa miradi hiyo haukubaliki.

Amesisitiza kuwa kukamilika kwa wakati kwa miradi hiyo si hisani bali ni wajibu wa kila mkandarasi aliyeaminiwa kutekeleza mradi kwa manufaa ya umma.

Mkuu huyo wa Mkoa ametembelea miradi kadhaa ikiwemo ule wa soko la Majengo, ambapo ameeleza kuwa mradi huo ni muhimu katika kupunguza msongamano wa wafanyabiashara katikati ya jiji.

Amebainisha kuwa kukamilika kwake kutarahisisha shughuli za biashara, kuongeza mapato ya halmashauri na kuboresha usafi wa mazingira.

Senyamule pia amesisitiza umuhimu wa kujenga eneo la maegesho ya magari katika soko la Majengo ili kuondoa usumbufu kwa wateja na wafanyabiashara watakaokuwa wakitumia soko hilo.

Aidha amemtaka mkandarasi wa ujenzi huo kuhakikisha mpangilio wa eneo hilo unazingatia mahitaji ya huduma za kijamii na urahisi wa upatikanaji wa bidhaa.

Kuhusu miradi ya barabara na madaraja, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ameeleza kuwa kukamilika kwake kutasaidia kuondoa adha ya mafuriko yanayojitokeza kila msimu wa mvua za masika, hivyo kuwezesha wananchi kusafiri na kufanya biashara bila vikwazo.

Amesema miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha mandhari ya jiji na kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Alhaj Jabir Shekimweri, amesema Serikali ya Wilaya itaendelea kuimarisha usimamizi wa miradi yote ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na wananchi wananufaika moja kwa moja na miradi hiyo.

Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya viongozi wa Serikali na wananchi ni nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Naye Mratibu wa Miradi ya TACTIC, Mhandisi Nicodemo Kileo, amesema miradi inayoendelea kutekelezwa Jijini Dodoma inagharimu zaidi ya shilingi bilioni 30 hadi kukamilika kwake.

Amebainisha kuwa miradi hiyo imekusudiwa kuboresha miundombinu ya biashara, usafiri na huduma za kijamii, sambamba na kuinua uchumi wa wananchi wa Dodoma.