Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TAASISI ya Everlasting Legal Aid Foundation (ELAF) imewataka Watanzania kuendeleza misingi ya amani, uvumilivu na maridhiano baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 7, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa ELAF, Dkt. Khamis Masoud, amesema kuwa uchaguzi umemalizika na sasa ni wakati wa viongozi na wananchi kushirikiana katika kujenga taifa lenye umoja, haki na utulivu.

“Tunapojenga amani, tunapanda mizizi ya ustaarabu, tunapochochea hasira, tunavuna majivuno ya kihistoria. Huu ni muda wa busara na maridhiano, si wa lawama,” amesema Dkt. Masoud.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo inaendelea kuhimiza viongozi wa kisiasa, wa dini na wa kijamii kutumia lugha za maridhiano badala ya kauli zinazoweza kugawa taifa, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu Katiba na utu wa kila Mtanzania.
Kwa mujibu wa taarifa ya ELAF, jamii bado inahitaji kuponya majeraha ya maneno, misuguano na tofauti zilizojitokeza wakati wa kampeni na uchaguzi, na njia pekee ni kuendelea kujenga imani na upendo miongoni mwa wananchi.
“Sheria inakuwa nuru inapolinda wote kwa usawa. Tunawasihi viongozi wote na wananchi wajiepushe na matamko yanayoweza kuibua hisia au kuchochea mgawanyiko. Amani ndiyo urithi wetu wa pamoja,” amesema.

Aidha, amesisitiza kuwa vyombo vya dola vinapaswa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kwa uwazi, kuhakikisha haki na ulinzi wa raia wote bila upendeleo.
Ametoa wito kwa serikali na viongozi wa dini kuhimiza mazungumzo ya maridhiano na mshikamano wa kitaifa, Vyombo vya habari kutumia kalamu zao kueneza amani na sio chuki.
“Vyombo vya usalama kuhakikisha ulinzi wa raia wote bila upendeleo, vijana kujitenga na maandamano, vurugu pamoja na mashirika ya kiraia kushiriki katika mijadala ya upatanisho wa kitaifa,” amesema.
Pia amekumbusha falsafa ya Kiafrika ya Ubuntu inayosisitiza heshima na utu wa kila mtu, ikisema taifa lenye amani linajengwa kwa kuamini kuwa “mimi ni kwa sababu sisi tupo.”
“Tanzania haina mbadala wa amani. Kila Mtanzania ana jukumu la kulinda misingi ya haki, upendo na umoja. Wakati wa uchaguzi umepita, sasa ni wakati wa kazi, busara na maridhiano,” amesema.



