Na Dotto Kwilasa, Jamhuri Media, Dodoma

Aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge lililopita na Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azan Zungu, ameibuka kidedea baada ya kuchaguliwa kwa kishindo kuwa mgombea wa nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika uchaguzi huo uliofanyika leo Novemba 9, 2025, jijini Dodoma, Zungu alipata kura 348, akimshinda mpinzani wake Stephen Masele aliyepata kura 16 pekee.

Kwa upande wa nafasi ya Naibu Spika, Mbunge Daniel Silo ameibuka kinara baada ya kupata kura 362, huku wagombea wengine waliokuwa wamejitokeza awali wakijiondoa kabla ya zoezi la upigaji kura kuanza.

Taarifa zinaeleza kuwa uchaguzi rasmi wa Spika na Naibu Spika unatarajiwa kufanyika Jumanne ijayo, ambapo CCM itapeleka jina lake lililopitishwa na vyama vingine navyo vitapendekeza wagombea wao endapo watakuwepo.

Uchaguzi huu ni hatua muhimu kuelekea kuundwa rasmi kwa uongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatua inayotarajiwa kufungua ukurasa mpya wa majadiliano na uwakilishi wa wananchi katika kipindi kipya cha uongozi.