Na Kija Elias, JakhuriMedia, Moshi

Shirika lisilo la kiserikali la Foundation for Community Transformation in Kilimanjaro (FTK), linalojihusisha na shughuli za maendeleo ya jamii, limeanzisha mpango maalumu wa kuelimisha watumishi wa umma na wanajamii kuhusu masuala yanayohusiana na afya ya akili.

Mpango huo, unaotekelezwa kupitia mafunzo ya siku nne, unalenga kuwaelimisha washiriki jinsi ya kushughulikia changamoto zinazohusiana na afya ya akili katika ngazi mbalimbali za jamii.

Akizungumza jana wakati wa semina hiyo iliyofanyika ukumbi wa TPC Mtendaji Mkuu wa FTK, Lazaro Urio, alisema mpango huo umeanzishwa kutokana na ongezeko la changamoto za afya ya akili miongoni mwa viongozi na wananchi katika maeneo ya vijijini.

“Utafiti uliofanywa na FTK katika wilaya ya Moshi umebaini kuwa viongozi wengi katika ngazi za vijiji na kata wanakabiliwa na changamoto katika kuhudumia watu wenye matatizo ya afya ya akili hivyo, tuliamua kuandaa programu hii kuwapa uelewa na mbinu za kushughulikia changamoto hizo,” alisema Urio.

Aliongeza kuwa semina hiyo imeandaliwa kwa ushirikiano na wataalamu wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC-ZRH) na wataalamu kutoka nchini Uholanzi.

“Mara nyingi mtu anapokabiliwa na matatizo ya kisaikolojia, hukimbilia kwa viongozi wa serikali au wa dini, kupitia mafunzo haya, viongozi hawa watakuwa na uwezo wa kuwasaidia watu kama hao ipasavyo,” alifafanua.

Urio alisema matarajio ya FTK ni kupanua huduma hiyo ya elimu kwa maeneo mengine ndani na nje ya mkoa wa Kilimanjaro, ili kuongeza uelewa kuhusu afya ya akili nchini.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi (DMO), Dk. Juma Mombokaleo, aliipongeza FTK, KCMC na wataalamu kutoka Uholanzi kwa kuanzisha programu hiyo, akisema inaunga mkono juhudi za serikali katika kushughulikia changamoto za afya ya akili.

“Serikali ya wilaya ya Moshi itatoa ushirikiano wa karibu kuhakikisha programu hii inakuwa endelevu, kwa kuwa afya ya akili ni msingi wa ustawi wa jamii,” alisema Dk. Mombokaleo.

Naye Mkuu wa Idara ya Saikolojia na Afya ya Akili wa KCMC, Dk. Kim Madundo, alisema takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya wanne anakabiliwa na changamoto za afya ya akili, huku zaidi ya Watanzania milioni saba wakiwa wanapata matatizo hayo.

“Wengi wao ni wale wanaokabiliana na changamoto za maisha kwa muda mrefu bila kupata suluhisho, elimu kama hii itawasaidia kujua namna ya kukabiliana na hali hizo,” alisema Dk. Madundo.

Kwa upande wake, mtaalamu wa afya ya akili kutoka Uholanzi, Dk. Rolf Schwarz, alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu hiyo mapema kwa vijana mashuleni.

“Vijana ni nguvu kazi na tumaini la taifa. Kuwafikia wakiwa bado shuleni kutasaidia kujenga jamii yenye afya bora ya akili kwa vizazi vijavyo,” alisema.