Na Manyerere Jackton, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mama Tanzania analia. Sauti yake haina maneno, lakini kila anayejua kusikia huzuni anaweza kuisikia kwa undani.
Ni kilio cha nchi iliyowahi kuwa mfano wa amani, heshima na utu barani Afrika, sasa ikikabiliwa na jeraha la damu ya watoto wake waliopoteza maisha mikononi mwa wenzao, mikononi mwa vyombo vilivyokusudiwa kuwalinda, mikononi mwa hasira na uamuzi wa haraka usio na busara.
Miaka michache iliyopita, Tanzania ilikuwa na sifa ya kipekee. Nchi iliyoishi kwa maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere: “Binadamu wote ni sawa, na uhai wa mtu ni mtakatifu.”
Leo, tunaposikia simulizi za mama anayeomboleza kijana wake aliyeuawa kwenye maandamano; mzee anayelalamika kuwa polisi walifyatua risasi hovyo; au kijana anayehofia hata kuzungumza hadharani kwa woga wa kupotea, tunajiuliza: Nini kimetupata?
Ni rahisi kulaumu upande mmoja, lakini ukweli ni mchungu — tatizo ni letu sote. Ni taifa zima lililopoteza maadili, utulivu wa fikra, na uvumilivu wa kijamii.
Katika miaka ya hivi karibuni, Watanzania mamia wamepoteza maisha katika matukio ya ghasia, mapambano ya kisiasa, vurugu za mitaani, au operesheni za usalama ambazo mara nyingine zimegeuka kuwa mauaji ya raia wasio na hatia.
Katika Jiji la Dar es Salaam, vijana waliokuwa wakishiriki maandamano ya kisiasa au ya kijamii waliishia kupigwa, kutupwa rumande, wengine kupotea kabisa. Wazazi waliwatafuta bila majibu. Kwenye mitaa ya Mbagala, Temeke, na Kinondoni, vilisikika vilio vya familia zilizopoteza ndugu zao.
Mashahidi wanasema risasi zilifyatuliwa bila tahadhari, wengine wakieleza waliona watu wakianguka huku wakipumua pumzi zao za mwisho. Haya yote yalifanyika katika ardhi ileile tuliyoapa kuilinda kwa jina la amani.
Nako Mwanza, jiji la Ziwa Victoria, hali haikuwa tofauti. Vijana waliokuwa wakikusanyika kupaza sauti zao juu waliambulia virungu na risasi. Wapo walioripotiwa kupoteza maisha, na wengine kujeruhiwa kiasi cha kubaki na ulemavu wa kudumu.

Mwanamke mmoja, mama wa watoto watatu, anasimulia kwa machozi jinsi mwanawe alivyotoka nyumbani asubuhi akisema anakwenda kushiriki maandamano ya amani, lakini hakurudi tena.
Alimpata hospitalini akiwa amekufa, akiwa amepigwa risasi kifuani. “Nilimwambia asiende,” anasema mama huyo, “lakini alisema, mama, hatuwezi kuishi kwa woga kila siku. Sasa niko peke yangu.”
Mtwara nayo haijanusurika. Katika miaka ya nyuma, mji huo ulishuhudia vurugu kubwa zilizohusiana na masuala ya gesi.
Polisi walitumia nguvu, wananchi wakapoteza maisha. Wengine waliishia kifungoni, wengine walipoteza makazi. Mahakama ziliwahi kushughulikia baadhi ya kesi, zikitoa hukumu kwa askari waliohusika, jambo lililotoa funzo na matumaini kwamba haki bado inaweza kupatikana, lakini kwa wengi, maumivu yalikuwa tayari yamezidi.
Na huko Tarime, eneo lenye historia ya migogoro ya kijamii na kiusalama, simulizi za vifo vya raia katika mikono ya vyombo vya dola si mpya. Safari hii watu kadhaa wameripotiwa kuuawa, na wengi kujeruhiwa.
Wakazi wanazungumza kwa hofu, wakihofia kulalamika zaidi. Haya yote yamekuwa sehemu ya kumbukumbu nyeusi kwenye historia yetu ya taifa lililojengwa kwa misingi ya utu na usawa.
Wengine wanasema tatizo si polisi wote, bali mfumo unaowatuma bila utaratibu, bila kuwapa elimu ya maadili na udhibiti wa nguvu. Polisi ni binadamu. Wanapokuwa chini ya shinikizo, bila mwongozo wa kimaadili, nguvu hubadilika kuwa ukatili. Hivyo, tatizo ni kubwa kuliko risasi — ni mfumo unaoruhusu risasi kufyatuliwa bila kuhesabu roho.
Katika kila kifo cha Mtanzania, iwe cha kijana, mwanamke, mzee au mtoto, kuna simulizi moja ya huzuni na hasara. Kila mwili unaolala chini ni mwito wa uhai uliokatishwa mapema. Mama analia, baba anafadhaika, jamii inakosa imani. Tunapopoteza mmoja wetu, tunapoteza nguvukazi katika Tanzania yetu.
Lakini licha ya haya yote, bado kuna tumaini. Tumaini hilo liko ndani ya moyo wa kila Mtanzania anayeamini kwamba damu haipaswi kumwagika tena, kwamba taifa letu linaweza kujirekebisha.

Hatua ya kwanza ni kukiri kwamba tuna tatizo. Tumezoea kusema “Tanzania ni nchi ya amani,” lakini amani si maneno; ni matendo. Amani haiwezi kuishi kwenye ardhi yenye woga, mateso, au unyanyasaji. Amani ni matokeo ya haki.
Haki ikipotea, amani huanza kuyumba taratibu. Na ndivyo ilivyotokea. Tulipoanza kukubali watu kufungwa bila sababu, tulipoanza kushangilia mateso ya wengine kwa kisingizio cha “wanastahili,” ndipo tulianza kuua roho ya utu ndani yetu.
Ni wakati sasa wa kurejea kwenye misingi ya taifa letu. Tanzania ilijengwa juu ya maridhiano na upendo. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema: “Kama huna amani, huna chochote.”
Sasa tunapaswa kuuliza: je, bado tuna amani? Je, bado tunaweza kukaa mezani — wapinzani na wanaotawala, vijana na wazee, raia na askari — na kuzungumza kwa heshima na upendo kama ndugu wamoja?
Kurejesha amani na maridhiano mapya si jambo la maneno matupu. Linahitaji hatua za makusudi. Kwanza, tunahitaji ukweli. Ukweli kuhusu nini kilitokea, nani alihusika, na kwanini.
Taifa haliwezi kupona bila kukabiliana na ukweli wake. Wapo walioumia, wapo walioua, wapo waliowapoteza wapendwa wao. Kila upande una uchungu. Hivyo, tunahitaji ‘tume huru ya ukweli na maridhiano’, kama ilivyofanyika Afrika Kusini baada ya ubaguzi wa rangi.
Ni njia pekee ya kutuliza roho za walioteseka na kuwapa matumaini wale waliobaki.
Pili, tunahitaji mabadiliko ya kimfumo katika vyombo vya ulinzi. Askari wanapaswa kupewa elimu ya kina ya maadili, uvumilivu, na haki za binadamu. Wanapaswa kufundishwa kuwa nguvu ni suluhisho la mwisho, si la kwanza.
Polisi anapolinda maandamano ya raia, hapaswi kuwa adui, bali mlezi wa usalama wa wote. Kila askari anayevunja kiapo cha kulinda maisha lazima awajibishwe kwa uwazi ili jamii irudishe imani.
Tatu, tunapaswa kuwekeza katika maridhiano ya kijamii. Vijana wasione silaha au vurugu kama njia pekee ya kusikika. Wananchi waone serikali yao kama mama, si adui. Hili linahitaji mazungumzo mapya ya taifa.
Serikali, vyama vya siasa, viongozi wa dini, wazee wa kimila, mashirika ya kiraia na wananchi waketi pamoja kujadili mustakabali wa taifa letu. Wote wana deni kwa Mama Tanzania.
Kwa sasa, tunaishi katika wakati ambao maneno ya faraja hayatoshi. Tunahitaji vitendo. Tunahitaji kuona machozi ya mama wa Mwanza yakifutwa, sauti ya kijana wa Kigoma ikisikika, na matumaini ya baba wa Tarime yakirejea.

Tunahitaji taifa linalosamehe, lakini lisilosahau; taifa linaloweka uwazi mbele, lakini likilinda heshima ya raia wake.
Uchumi unaweza kukua, barabara zikajengwa, majengo yakasimama, lakini ikiwa tunapoteza utu — basi tumepoteza kila kitu.
Uhai wa mwananchi mmoja ni thamani isiyopimika kwa fedha wala mamlaka. Kifo cha raia mmoja kisichukuliwe kama takwimu, bali kama ishara ya udhaifu wa mfumo wetu.
Leo, Mama Tanzania anapumua kwa shida. Alishuhudia watoto wake wakiuana, akalia kuona damu ikitiririka mitaani. Lakini bado ana moyo wa msamaha. Anatuomba, sio kwa nguvu, bali kwa upendo: “Watoto wangu, rudisheni amani nyumbani.”
Huu ni mwito kwa viongozi wote — wa kisiasa, wa dini, wa kijamii na wa vyombo vya dola — kutambua kwamba mamlaka bila maadili ni hatari. Ni wakati wa kuchagua busara kuliko nguvu, mazungumzo kuliko risasi, uhai kuliko ushindi wa kisiasa.
Tanzania tuliyoizoea — ile ya nyimbo za amani, ya jirani anayemsaidia jirani, ya wazee wanaokemea vita — bado inaweza kurejea. Tunachohitaji ni ujasiri wa kukiri makosa, kusamehe, na kujenga upya imani iliyopotea.
Kizazi kipya cha Watanzania kina haki ya kurithi nchi yenye amani na haki. Haki ambayo haijengwi kwa hofu, bali kwa ukweli. Amani ambayo haidumu kwa woga, bali kwa uelewa wa pamoja.
Mama Tanzania hawezi kufurahia hadi atakapoona watoto wake wanakaa mezani, wanazungumza kwa upendo, na wanaheshimiana tena. Tukirudisha utu, tutakuwa tumerudisha amani. Tukijenga maridhiano, tutakuwa tumejenga mustakabali wa kweli. “Amani ni matokeo ya haki. Bila haki, hakuna amani.” J.K Nyerere (Jarida la Alliance, Juni 1, 1998).
Wakati umefika wa kutibu jeraha hili. Wakati umefika wa kusikilizana, si kushindana. Wakati umefika wa kuandika ukurasa mpya wa historia yetu — ukurasa wa maridhiano, haki na amani.
Mama Tanzania anatuangalia. Ana macho yenye matumaini, licha ya machozi yake. Swali ni moja tu: tutamfanya atabasamu tena, au tutaendelea kumfanya alie?
Naam, bado tunayo nafasi ya kumfuta machozi! Naye anasema, “Mimi ni Mama Tanzania. Nimewapokea mlipotoka mbali, nikiwaangalia mkikua katika ardhi yangu yenye rutuba na jua la matumaini. Nimefurahia mkiimba nyimbo za umoja, nikahuzunika mlipogeukiana kwa hasira na visasi. Lakini bado nawathamini nyote — walio hai na waliolala kaburini kwa mikono ya wenzao.
“Sitaki kulia tena, watoto wangu. Nataka kuona mkipeana mikono, mkijenga madaraja ya imani, mkisamehe, mkianza upya. Amani yangu si zawadi ya kisiasa, ni urithi wa damu zenu na jasho lenu.
“Mkinisikiliza, mtasikia pumzi yangu ikisema taratibu: Tanzania, amka upya. Sio kwa chuki, bali kwa maridhiano. Sio kwa visasi, bali kwa huruma. Na wakati huo, nitapumua tena kwa furaha, nikiitazama nchi yangu ikirudia kuwa kimbilio la upendo, haki na utu.”
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Ibariki Afrika.
0759 488 955


