Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemuapisha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla iliyofanyika Novemba 14, 2025, Ikulu Chamwino, Dodoma.

‎Akitoa maelekezo baada ya kumwapisha, Rais Dkt. Samia amesema kuwa uteuzi wa Dkt. Nchemba umezingatia uwezo wake wa kuitumikia nchi na kusimamia masuala ya msingi kwa maslahi ya wananchi. Amesema kuwa majukumu yake yote yako ndani ya Katiba na kwamba amemkabidhi vitabu vinavyoeleza wajibu wake kama kiongozi mkuu wa Serikali bungeni.

‎Aidha, Dkt .Samia amebainisha kuwa Serikali ina muda mfupi wa kutekeleza ahadi za Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025, hivyo kasi ya utendaji lazima iongezwe. Amesema kuwa jukumu kubwa la Dkt. Nchemba sasa ni kuliongoza Baraza la Mawaziri na kuhakikisha kila sekta inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi ndani ya muda uliopangwa.

‎Aidha, Rais Dkt. Samia amesema kuwa utekelezaji wa miradi na mipango ya Serikali unategemea upatikanaji wa fedha, na kwa kuwa Dkt. Nchemba amekuwa sehemu ya mfumo wa kusimamia uchumi kwa miaka mitano, anatakiwa kuhakikisha taratibu hizo zinaendelezwa bila kupungua kwa kasi.

‎Amesema kuwa Dkt. Nchemba ana mzigo mkubwa unaohitaji nidhamu, uadilifu na uthubutu, akisisitiza kuwa majukumu hayo yanahitaji kiongozi ambaye yuko tayari kusimamia maslahi ya taifa bila kuyumbishwa na vishawishi.

‎Aidha, amebainisha kuwa nafasi ya Waziri Mkuu ni nyeti na haiendeshwi kwa misukumo ya marafiki au jamaa, bali kwa kutanguliza maslahi ya Watanzania.