Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Isimani mkoani Iringa, William Lukuvi, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hajakosea kumteua Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, akibainisha kuwa ni kiongozi mwenye weledi, uzoefu mpana na uadilifu wa hali ya juu katika utumishi wa umma.
Lukuvi, mmoja wa wanasiasa wenye uzoefu mkubwa ndani ya Bunge la Tanzania, amesema ubobevu wa kitaaluma wa Dkt. Mwigulu ni uthibitisho wa uwezo wake wa kipekee, akitaja uzoefu wake wa kufanya kazi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kabla ya kuingia kwenye siasa kama nguzo muhimu inayomuandaa kuwa kiongozi makini.
Ameongeza kuwa Dkt. Mwigulu ana historia ndefu ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambako amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu, Mjumbe wa Kamati Kuu, Mjumbe wa Sekretarieti, na Naibu Katibu Mkuu wa CCM kati ya mwaka 2012 hadi 2015 nafasi ambazo zimemjengea uzoefu na maono ya kisiasa yenye tija kwa taifa.
Leo, Alhamisi Novemba 13, 2025, Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemthibitisha rasmi Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu kwa kura 369 kati ya kura 371 zilizopigwa, huku kura mbili zikiharibika.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Waziri Mkuu mteule ataapishwa kesho Ijumaa, Novemba 14, 2025, katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, kuanza rasmi majukumu yake mapya.


