Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mwigulu Nchemba, amefanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya rufani ya Mkoa wa Dodoma na kupiga marufuku tabia ya kuwasubirisha wajawazito mapokezi wakiwa na uchungu wa kujifungua.

Ziara hiyo inakuja ikiwa ni siku moja tangu Dk.Nchemba aapishwe kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Samia Suluhu Hassan, juzi Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Akiwa kwenye ziara hiyo leo November 15,2025 Dk.Nchemba amepata fursa ya kuzungumza na watumishi, wagonjwa pamoja na ndugu na jamaa wa wagonjwa walifika hospitalini hapo.

Akizungumza na wagonjwa, aliwahoji namna ambavyo wamekuwa wakipatiwa huduma za matibabu na watumishi walipo katika hospitali hiyo.

Mara baada ya kumaliza kukagua utoaji huduma katika hospitali hiyo, alitoa maagizo kadhaa kwa hospitali zote nchini ikiwamo kuacha tabia ya kuwasubirisha mapokezi wajawazito wenye uchungu wa kutaka kujifungua.

“Maagizo yangu ni kwamba na hii ni kwa ajili ya hospitali zote nchini kuwa ni marufuku wajawazito kusubirishwa mapokezi kwa ajili ya kuandikishwa bali wapate huduma kwanza na anayehitaji kuwaandikisha awafute huko wodini,”alisema

Pia, alisema wakati akizungumza na wagonjwa kwenye hospitali hiyo amebaini ipo changamoto ya wajawazito kutohudumiwa kwa kukosa ndoo ama beseni.

Alisema, siyo jambo jema kwa mama mjamzito ambaye anahitaji kujifungua kuzuliwa kwakukosa ndoo au beseni bali hospitali zote zinapaswa kuwa na vifaa hivyo kama dharura kwa wale wasiyo kuwanavyo.

“Hospitali inapaswa kuwa na ndoo na beseni za ziada kwa ajili ya kusaidia hawa ambao hawana vifaa hivyo wakati huu ambapo serikali inaendelea kushughulikia suala la bima ya afya kwa wote,”alisema Dk. Nchemba

Aidha, aliziagiza hospitali zote nchini Wizara ya Afya pamoja na Bohari ya Dawa nchini (MSD), kuweka vipaumbele vya kununua dawa kutokana mahitaji ya eneo husika.

Alisema, hivi sasa kumekuwepo na tabia hospitali za serikali kutumika kwa ajili ya kutoa vipimo, lakini inapofika suala la dawa wagonjwa wanaambiwa wakanunue maduka ya nje.

“Kama hospitali ya serikali inakosa dawa duka la nje linapataje dawa hiyo hii ni tabia ya baadhi ya wataalam kuagiza panado kwenye hospitali za umma wakijua watawaambia wagojwa wapi pa kuipata dawa hiyo muhimu kwenye vioski vya nje,’alisema

Alisema, Rais Samia Suluhu Hassan, ametumia kiasi kikubwa cha fedha kwenye vifaa tiba na dawa haiwezekani hospitali ya umma ikakosa dawa wakati maduka binafsi zinakuwepo.

“Rais ametumia fedha nyingi kwenye vifaa na dawa hatuwezi kuendelea kuwa na uhaba wa dawa wakati maduka binafsi zipo kama wewe serikali unakosa binafsi wanapata wapi hivyo niagize jambo hili lifanyiwe kazi katika hospitali zote nchini,”alisema

Hata hivyo, alielezwa kuridhishwa na namana hospitli hiyo imekuwa ikitoa huduma kwa wananchi na kuagiza changamoto zilizopo kufanyiwa kazi.


Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Ibenzi Ernest alimshukuru Waziri Mkuu kwa kuchagua kituo chao na kufanya ziara ya kugaua utoaji huduma za matibabu kwa wananchi.