Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Singida

Leo nimesali jijini Dar es Salaam. Mara tu baada ya misa nikasafiri kuja hapa Singida. Nashukuru ujio wa SGR na kuboreshwa kwa miundombinu, muda nilioutumia Dar es Salaam hadi Singida, zamani ilikuwa ndoto za alinacha. Leo kwa Tanzania yanawezekana.

Mtanisamehe kwa kuwa na kichwa cha habari kirefu katika makala hii ya SITANII; Nimewasikia Rais Samia, Maaskofu, BAKWATA, nashauri tuienzi busara ya mfalme Suleiman.

Sitanii, wiki iliyopita Rais Samia Suluhu Hassan amezindua Bunge la 13 jijini Dodoma. Amewateua Mwanasheria Mkuu, Hamza Johari na Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba. Nimegushwa na hotuba aliyoitoa Rais Samia bungeni, ambayo imeeleza mengi, lakini kubwa dhana ya maridhiano na kuwapa fursa vijana kwa kiwango cha kuwaundia wizara kamili ya vijana.

Rais Samia amemsihi Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, awafutie mashitaka ya uhaini vijana walioshiriki maandamano. Ametoa pole kwa Watanzania waliofariki, walioumia na ambao wamepoteza mali. Mwisho amesema serikali yake haitachoka kunyoosha mkono wa maridhiano.

Sitanii, nafahamu Rais Samia anaposema ‘kunyoosha mkono wa maridhiano’, nakumbuka ukweli kwamba Desemba 23, 2021, aliunda Kikosi Kazi cha Hali ya Siasa nchini. Vyama 18 vyenye usajili wa kudumu vilikubali kutoa maoni mbele ya Kikosi Kazi hiki, isipokuwa chama kimoja tu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Hoja yao ilikuwa ni kuwa wao ni chama kikuu cha upinzani nchini, hawawezi kuchanganywa na vyama vingine vidogo.

Rais Samia hakuwagomea. Alikubali kukutana na CHADEMA. Wakawa na mazungumzo ya kando na Kikosi Kazi. Kama sehemu ya maridhiano siku chache baadaye, yaani Machi 8, 2023 alihudhuria mkutano wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA), Moshi, mkoani, Kilimanjaro. Nako alitangaza maridhiano na nchi ikawa pamoja. Baadaye CHADEMA wakajitoa katika maridhiano. Sasa si wakati wa kulijadili hili.

Sitanii, nimesema nimemsikia Rais Samia, lakini pia wengine niliowasikia ni maaskofu wa Kanisa Katoliki, kupitia Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC). Nikiri mimi ni Mkatoliki. Sisi tumekuzwa na kulelewa katika utii. Na hapa sitavunja hili agano, bali nitashauri. Nimeyasikia mambo makuu manne hivi, waliyosema maaskofu wetu. Wanapinga watu kuuawa au kupotezwa na watu wasiojulikana. Hili niliishaliandika. Nami nalipinga.

Si mimi tu, hata Rais Samia Juni 27, 2025 wakati anatoa hotuba ya kuvunja Bunge la 12, aliwaagiza polisi kuwa hataki kusikia mtu anapotea. Tangu wakati huo, kumbukumbu zangu zinanionyesha hakuna Mtanzania aliyeripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Hili nimesema imekuwa ni kero kubwa inayostahili kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Watu wasiojulikana, watafutwe hadi wajulikane na kuwajibishwa. Ndiyo maana tunalipa kodi kwa ajili ya ulinzi wa maisha yetu na mali.

Jambo la pili, maaskofu Katoliki wamesema kwa muda mrefu tangu mwaka 2016 uchaguzi si huru wala wa haki. Huu umekuwa mjadala wa muda mrefu na watu wengi hapa nchini, nikiwamo mimi tunaukataa mfumo wa vyama vya upinzani kuambiwa hawajui kusoma na kuandika, isipokuwa wa chama tawala ilihali wote wamesoma darasa moja. Ni lazima tuwe na mfumo wa uchaguzi unaompa ushindi aliyeshinda, si aliyeamuriwa kushinda. Si tu haki itendeke, bali ionekane kutendeka.

Sitanii, jambo la tatu na kubwa lililozungumzwa na Maaskofu Katolilki kupitia TEC, wamependekeza viongozi wa vyombo vya dola wawajibike. Mimi ni nani basi hata nitie neno katika hili? Jingine la nne, ambalo wamelitaka ni chombo cha uchunguzi kutoka Jumuiya ya Madola. Binafsi sitayajadili haya mawili, ingawa hili la chombo huru kutoka nje kwa pamoja tusome Mkataba wa Vienna wa mwaka 1963 juu ya mamlaka ya nchi, nadhani ni gumu kutekelezeka. Ila nieleweke mababa sijawapinga, nawapa taarifa.

Jambo moja naliona ugumu ni hii kazi ya uandishi wa habari. Yaani kama Pilato alivyonawa mikono katika kumhukumu Yesu, kazi yetu inatupasa kusema ukweli, ili ukweli ubaki katika kumbukumbu. Hili si jingine, bali niseme nasikitika kuwa Watanzania wenzetu wamepoteza maisha. Sote tunalia machozi yanatutoka.

Ninaposema Watanzania najumuisha vijana waliokuwa wanaandamana, polisi waliokuwa kwenye lindo na askari mgambo waliokuwa wanalinda vituo vya kura. Zipo taarifa za wasimamizi wa uchaguzi ambao ama waliumia au walifia kwenye vituo vya kura na ofisi zilizochomwa moto. Hawa nao ni binadamu, ni Watanzania wenzetu. Kitambo sasa kama nchi na kimataifa tunabishania idadi ya waliokufa. Maneno yaliyobaki kutumika ni wamefariki wengi.

Wakati natafuta taarifa ameniuliza swali mtu mmoja, kwamba kuna mtaa wowote ambao nimekuta nyumba 10 au 20 zimeweka matanga kwa kufiwa na ndugu katika maandamano haya? Hao wengi ni wangapi na wako wapi? Mimi sina jibu katika maswali haya, ila nasema hata kama ni mmoja hakupaswa kupoteza maisha, lakini pia si sahihi kutumia neno ‘wengi’ kama blanketi kuhalalisha ajenda ya kimataifa.

Wakati nikiwa katika masikitiko ya vijana kupoteza maisha, niseme nimesikitika kuona maaskofu kutoka TEC tamko lao halikuwa na msitari hata mmoja kuwaonya Gen-Z walioua, kupora au kuteketeza mali za watu kwa moto. Kumbe wanaweza kuona wamepewa ruzuku ya kutetewa hata Desemba 9, 2025 wakaingia barabarani tena, si kuandamana, bali kufanya maafa.

Nilidhani TEC ilikuwa na wajibu wa kuwatahadharisha vijana kuandamana bila kufanya uhalifu. Kwa utii naishia hapo.

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) nao wametoa tamko lao ila wao wameanza kwa kutangaza maombi kwa taifa. Wametangaza siku kuombea waliopoteza maisha, walioumia, mahakama, serikali na viongozi mbalimbali. Mwisho, wametoa wito kwa serikali kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya wananchi sawa na walivyosema TEC, wameitaka serikali kutenda haki kwa waliopoteza maisha na walioathirika.

KKKT wameisihi serikali na vyombo vya dola kuepuka matumizi ya nguvu kupita kiasi hasa risasi za moto. KKKT nao hawakuwagusa wanaharakati walioko nje ya nchi wanaohamasisha maandamano, wala vijana walioandamana kuwaasa jinsi ya kuandamana bila kupora mali za watu, kuchoma na kutesa waliopiga kura. Nadhani kama nilivyowaasa maaskofu wa TEC, basi na hapa nishauri tu, kuwa vijana walioshiriki maandamano, pamoja na maandamano kuwa haki yao, walistahili neno pia.

Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) nao wametoa tamko. Hawa wamehimiza amani, mshikamano, kuwaombea waliofariki au kuumia, lakini pia wakakemea waandamanaji kwa vitendo vya uporaji na uharibifu wa mali za watu binafsi na umma. BAKWATA nao hawakuigusa serikali hata chembe juu ya matumizi ya nguvu kupita kiasi, nilidhani tamko lao nao lilipaswa kuligusa hili.

Sitanii, kilichonitisha katika tamko la BAKWATA ni kauli kuwa hakuna dini bora zaidi ya nyingine au raia daraja la pili au kwamba wao wasichukuliwe kuwa hawana akili na baadhi ya dini. Hapa nimeogopa. Nimeona maandalizi ya mabishano yanayoweza kuzaa vita ya kidini ambayo ni hatari zaidi kuliko hii ya Gen-Z. Nawashukuru BAKWATA wamewakemea watu kutoka nje ya nchi wanaohamasisha vurugu, ila mkondo wa dini kutiliana shaka umeniogopesha.

Lakini niwashirikishe jingine, maana safu hii inakuwa fupi. Tunapaswa kuchukua hatua haraka kuliko tunavyodhani. Wiki iliyopita niliandika makala. Niligusa pande zote mbili; waandamanaji na serikali. Nimepokea simu nyingi zinazosema zamu hii wafanyabiashara hawatakubali kupoteza tena mali zao kama ilivyotokea Oktoba 29, 2025.

Wengi walionipigia wanasema waandamanaji wakiingia barabarani, wao watamalizana nao huko huko barabarani kabla hawajachepuka kufikia biashara zao mitaani. Tunaiona hatari hiyo? Kumbe kundi la wafanyabiashara ambalo ndani yake lina vijana, wakiamua kujibu mapigo, yatatokea maafa makubwa kuliko tuliyoyashuhudia. Wanasema watawawahi barabarani huko huko kabla hawajafikia biashara zao.

Sitanii, hali ndiyo hiyo tuliyonayo. Maandiko matakatifu yanaonyesha kina mama wawili walijifungua. Mmoja akapitiwa na usingizi akakilalia kichanga chake kikafa. Kuona vile, akapora kichanga kilicho hai na kudai ndicho chake. Kesi ikafika mbele ya Mfalme Suleiman. Mfalme Suleiman akawahoji wanataka iweje, kwamba wao ndiyo waiamue kesi hiyo.

Mama aliyelalia kichanga chake akawa wa kwanza kunena. Akasema kwa kuwa imekuwa vigumu kupata ufumbuzi bora kichanga kilicho hai kipasuliwe katikati kila mwanamama apewe kipande akazike. Mama wa mtoto halisi akaulizwa wazo hilo analionaje? Akasema kuliko kumpasua, bora huyo mama apewe mtoto aliye hai yeye atakuwa akimwona angalau wakati anapita njiani.

Mfalme Suleiman hakusita. Akakata shauri kwa kusema mama aliyekataa mtoto asipasuliwe vipande viwili ndiye mama halisi wa mtoto na hivyo akabidhiwe mtoto. Mbele yetu upo mtihani. Serikali, maaskofu, masheikh, wanaharakati, vyama vya siasa na yeyote awaye. Mtoto mmoja amefariki, amebaki mmoja Tanzania. Mtoto aliye hai Tanzania tunayo kazi ya kuamua iwapo tupasue vipande viwili kila mtu akazike au akabidhiwe kwa mama mwingine aendelee kuishi? Tuamue. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827