Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) wamepokelewa katika Ofisi za Wizara zilizoko Mji wa Serikali Mtumba baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Mhe. Balozi Kombo aliambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ng’waru Jumanne Maghembe (Mb) na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya (Mb) na kulakiwa na Viongozi na Watumishi wa Wizara waliokusanyika katika Ofisi hizo.

Akizungumza na Menejimenti ya Wizara Mhe. Waziri Kombo aliwashukuru viongozi wa Wizara na Watumishi kwa mapokezi waliyoyapata. Amesisitiza dhamira yake ya kuendeleza juhudi za Tanzania katika diplomasia na kuahidi kushirikiana na watumishi ili kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita kikamilifu.
Amewasihi watumishi kushirikiana, kupendana, kuwa wamoja na kushirikisha wengine wakati wa kutekeleza majukumu yao ili kuongeza tija na ufanisi.
“Watumishi muongeze vitu vinne katika kutekeleza majukumu yenu, muwe na ushirikiano, upendo, umoja na mshirikishe wengine katika kutekeleza majukumu yenu, mkizingatia hivyo kila kitu kitaenda sawa na mtakuwa mnatekeleza majukumu yenu kwa tija na ufanisi, ”

Wakizungumza katika kikao hicho Mhe. Naibu Waziri Mhe. Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe na Mhe. Naibu Waziri James Kinyasi Millya kwa pamoja walieleza utayari wa kushirikiana na watumishi wa Wizara kutekeleza majukumu yao ili kuwa na Tanzania imara yenye taswira nzuri wakati wote.
Mhe. Balozi Kombo pamoja na Naibu Mawaziri, Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe na Mhe. James Kinyasi Ole Millya wameapishwa Ikulu Chamwino baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika nyadhifa hizo baada ya kuunda Baraza Jipya la Mawaziri kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025.






