Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha programu maalum ya mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari kutoka mikoa mbalimbali, lengo likiwa kuongeza umahiri katika kuripoti masuala ya uchumi na fedha kwa usahihi na weledi.
Akizindua mafunzo hayo Jijini Dodoma leo November 19,2025 Meneja wa Huduma za Kibenki na Sarafu BoT, Nolasco Matuli, amesema semina hiyo imeandaliwa ili kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuelewa kwa undani jukumu la Benki Kuu, ikiwemo usimamizi wa sera za fedha, mzunguko wa uchumi, na umuhimu wa taarifa sahihi katika kuchochea maendeleo.

Amesisitiza kuwa uandishi makini wa masuala ya uchumi ni msingi muhimu katika kufanya maamuzi ya sera na biashara.
Matuli ameongeza kuwa mafunzo hayo yataimarisha pia ushirikiano kati ya BoT na vyombo vya habari, kwa kuweka mazingira ya mawasiliano ya karibu na kuboresha upatikanaji wa taarifa za kifedha kwa wananchi.
“Kupitia semina hii wanahabari mnatarajiwa kuwa na uwezo mpana wa kufasiri takwimu, kuelewa muundo wa sekta ya fedha na kuripoti kwa usahihi mwenendo wa uchumi, ” ameeleza.

Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa Uchumi BoT–Dodoma, Shamy Chamicha, amewasilisha mada kuhusu jukumu la Benki Kuu katika kulinda thamani ya shilingi, kudhibiti mfumuko wa bei na kusimamia sekta ya fedha.
Amebainisha kuwa sera ya fedha ndiyo injini inayowezesha uchumi kukua bila kuingia katika misukosuko, huku BoT ikihakikisha uthabiti wa mifumo ya malipo, utoaji wa leseni kwa taasisi za fedha na usimamizi wa amana za wananchi.
Chamicha amefafanua kuwa BoT ina jukumu pia la kusimamia usambazaji wa sarafu nchini na kuendeleza mifumo ya malipo ya kisasa ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama.
Amesema hatua hizo ni muhimu katika kukuza uchumi wa kidijitali na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kifedha zenye ubora na usalama.

Akizungumzia utekelezaji wa Sera ya Fedha kupitia matumizi ya riba, Chamicha alieleza kuwa nyenzo hiyo hutumika kudhibiti mzunguko wa fedha ili kuimarisha bei za bidhaa na huduma. Alisema riba inapopanda hupunguza matumizi na mikopo, hivyo kupunguza shinikizo la mfumuko wa bei, huku riba inaposhuka ikichochea uzalishaji na ukuaji wa uchumi.
Semina hiyo inaendelea jijini Dodoma hadi Novemba 21, ambapo washiriki wanatarajiwa kujifunza kwa kina kuhusu uchumi mpana, masoko ya fedha, usimamizi wa sera na mbinu sahihi za kutafsiri takwimu za kiuchumi kwa ajili ya umma.




