Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewaonya viongozi wazembe na wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, kikisisitiza kwamba hakitamvumilia kiongozi yeyote anayeshindwa kuwajibika kwa wananchi.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, amesema hayo leo Novemba 17,2025 Jijini Dodoma na kueleza kuwa chama kitaweka vipimo maalum vya kupima utendaji wa viongozi katika ngazi zote ili kuhakikisha uwajibikaji unazingatiwa kikamilifu.
“Mawaziri na Manaibu Mawaziri walioteuliwa na Rais wanapaswa kwenda sambamba na kasi ya utendaji ya kiongozi wa nchi,ingawa baadhi yao ni wapya na wanafurahia uteuzi, wanapaswa kufahamu kuwa Rais anataka kazi yenye matokeo kwa wananchi na hana mzaha katika masuala ya utumishi wa umma,” amesema Kihongosi.
Amesisitiza kuwa CCM haitasita kumchukulia hatua yoyote atakayekwenda kinyume na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Kihongosi amesema chama kipo bega kwa bega na Mwenyekiti wake, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuimarika nchini.
Kihongosi pia amewapongeza viongozi walioapishwa, wakiwemo Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, Dkt. Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Fedha, Mwiguru, akiwataka kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kuwatumikia wananchi kwa weledi.
Akizungumzia hatua ya Rais Samia ya kuomba vijana waliokamatwa kutokana na vurugu za Oktoba 29 waachiwe, Kihongosi amesema ni uthibitisho wa uongozi wa huruma na busara.
Pia ametoa pongezi kwa uundwaji wa timu maalum ya kuchunguza vurugu hizo, pamoja na ahadi ya Rais kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya ndani ya siku 100.
Aidha, Kihongosi alisema kuwa ndani ya siku 11, ajira zimeanza kutolewa na hospitali zimekatazwa kutoza malipo yasiyo rasmi, ikiwemo suala la kutoza fedha za kutuza maiti, huku akisisitiza kwamba wananchi wanapaswa kupata huduma stahiki bila usumbufu.



