Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BENKI ya CRDB imeweka historia katika masoko ya mitaji nchini baada ya kuiorodhesha rasmi hatifungani yake ya Kiislamu ya CRDB Al Barakah Sukuk katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hatua iliyoibua mwitikio mkubwa wa wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Uorodheshaji huo umefanyika huku benki hiyo ikitangaza kuvuka malengo ya mauzo kwa kukusanya Shilingi bilioni 125.4 na Dola za Marekani milioni 32.3, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa katika bidhaa za aina hiyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Novemba 19, 2025, katika Hafla ya kutangaza matokeo na kuorodheshwa kwa hatifungani hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Elijah Mwandumbya, amesema kuwa mafanikio hayo yanaonyesha kukua kwa masoko ya mitaji nchini.

Amesema Serikali inaendelea kuandaa sheria maalumu zitakazosimamia huduma za fedha za Kiislamu ili kuongeza uwazi na kuvutia wawekezaji wengi zaidi.

“Utendaji huu wa kipekee wa Sukuk hii ni uthibitisho tosha wa kulia kwa masoko ya mitaji nchini Tanzania na shauku kubwa ya wawekezaji kwa bidhaa bunifu za uwekezaji,” amesema Dkt. Mwandumbya.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema hatifungani hiyo imevutia zaidi ya wawekezaji 1,000 kutoka Tanzania na nchi saba nyingine, ikiwa ni pamoja na taasisi za dini, wawekezaji binafsi na wa kimataifa.

“Watanzania binafsi wamewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 70, huku zaidi ya Shilingi bilioni 50 zikitoka kwa wawekezaji wa kimataifa. Hii ni ishara ya kuongezeka kwa imani ya dunia kwa soko la mitaji la Tanzania,” amesema.

Kwa mujibu wa Nsekela, Sukuk hiyo ni sehemu ya mpango wa miaka mitano wa kukusanya Dola milioni 300 kwa ufadhili wa miradi ya maendeleo, kuongezea nguvu sekta ya biashara ndogo na za kati na kupanua ujumuishi wa kifedha.

Kwa upande wa mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Exaud Julius, amesema mauzo ya Sukuk yamechangia kuongeza thamani ya soko la hisa kutoka Shilingi trilioni 13.5 hadi trilioni 13.7, ikiwa ni uthibitisho wa kuongezeka kwa imani ya wananchi katika uwekezaji wa hatifungani za makampuni.

Mkurugenzi Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela, amesema uorodheshaji wa Sukuk hiyo unaimarisha nafasi ya Tanzania katika masoko ya kimataifa ya fedha yanayofuata misingi ya Kiislamu, akitaja kuwa kiwango cha mauzo kilichofikiwa kinaonyesha ubora wa mifumo ya udhibiti wa masoko ya mitaji nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB, Profesa Neema Mori, amesema mafanikio hayo yanatoa msukumo kwa benki kuendeleza bidhaa bunifu zenye maadili na zinazolenga makundi mbalimbali ya jamii.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Sharia, Abdul Van Mohammed, amesisitiza kuwa sheria mpya za fedha za Kiislamu zitakapoanza kutumika, Tanzania itapata fursa pana ya kuunganishwa na masoko yenye ukwasi mkubwa kama yale ya nchi za Ghuba.

Tangu kuanzishwa kwa huduma za Al Barakah mwaka 2021, CRDB imeshahudumia wateja zaidi ya 400,000 na kutoa uwezeshaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 287 katika miradi inayozingatia misingi ya Sharia.