*Ni mafanikio ya asilimia 646
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dar es Salaam
Benki ya CRDB imetangaza mafanikio ya kihistoria pamoja na kuiorodhesha rasmi hatifungani yake inayofuata misingi ya sharia ya dini ya Kiislamu ‘CRDB Al Barakah Sukuk’ katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hatua inayoweka rekodi mpya katika ukuaji wa masoko ya mitaji nchini. Hatifungani hii imevunja rekodi kwa kukusanya Shilingi bilioni 125.4 sawa na asilimia 418 ya lengo lililowekwa pamoja na dola za Marekani milioni 32.3 sawa na asilimia 646.
Akizunguimza katika hafla ya kutangaza matokeo na kuorodheshwa kwa hatifungani hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Elijah Mwandumbya ameipongeza Benki ya CRDB kwa mafanikio hayo na kuyaelezea kama hatua muhimu sana kwa taifa.

“Utendaji huu wa kipekee wa Sukuk hii ni uthibitisho tosha wa kukua kwa masoko ya mitaji nchini Tanzania na shauku kubwa ya wawekezaji kwa bidhaa bunifu za uwekezaji,” amesema Dkt. Mwandumbya.
“Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji ikiwamo kukamilisha sheria mahsusi za kusimamia huduma za fedha zinazofuata misingi ya Kiislamu ambazo zitaongeza uwazi, kuimarisha ulinzi wa wawekezaji, na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha ushindani wa huduma za fedha zinachozingatia misingi ya sharia Afrika,” amsema Dkt. Mwandumbya.
Akizungumza na wawekezaji waliojitokeza kushuhudia kuorodheshwa kwa CRDB Al Barakah Sukuk katika soko la hisa, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema matokeo haya yamevuka matarajio katika sarafu zote mbili ambazo wawekezaji waliruhusiwa kuwekeza. Amesema hatifungani hii imevutia zaidi ya wawekezaji 1,000 wakiwemo watu binafsi, taasisi, makundi ya kidini na wawekezaji wa kimataifa kutoka zaidi ya nchi saba.
“Tulichokishuhudia leo ni historia mpya. Kukusanya shilingi bilioni 125.4 na dola za Marekani milioni 32.3 si tu ushindi kwa Benki ya CRDB bali ni kielelezo cha imani kwa Tanzania.
Zaidi ya shilingi bilioni 70 zimewekezwa na Watanzania binafsi, ishara ya kuongezeka kwa uelewa wa masuala ya kifedha na kuaminika kwa masoko yetu. Na zaidi ya shilingi bilioni 50 zimetoka kwa wawekezaji wa kimataifa, kuthibitisha kuwa Tanzania sasa ni kivutio muhimu kwa uwekezaji wa huduma za fedha zinazofuata misingi ya Kiislamu,” amesema Nsekela.

Nsekela ameongeza kuwa hatifungani hii ya CRDB Al Barakah Sukuk ni mwendelezo wa mpango wa muda mrefu wa Benki wa kukusanya shilingi sawa na dola za Marekani milioni 300 katika kipindi cha miaka mitano ili kufadhili miradi ya maendeleo, kupanua utoaji wa mitaji kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), na kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Exaud Julius amesema mafanikio yaliyopatikana kwenye mauzo ya CRDB Al Barakah Sukuk yamechangiwa na sera endelevu za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini. “Kwa matokeo haya ni dhahiri imani ya wananchi kuwekeza kwenye hatifungani za makampuni imeongezeka,” amesema Julius.
Kwa kuiorodhesha CRDB Al Barakah Sukuk, Julius amesema thamani ya uwekezaji katika Soko la Hisa Dar es Salaam imependa mpaka shilingi trilioni 13.7 kutoka shiligi trilioni 13.5 na kuongeza idadi ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela amepongeza mafanikio ya hatifungani hiyo akisisitiza kuwa kiwango kikubwa cha mauzo kilichofanyika kinadhihirisha imani kubwa ya wawekezaji katika uimara wa mifumo ya udhibiti nchini.
“Kuorodheshwa kwake kutaimarisha ukwasi, kuongeza wigo wa ushiriki, na kuiweka Tanzania katika nafasi ya masoko ya kimataifa ya huduma za fedha zinazofuata misingi ya dini ya Kiislamu kama ilivyo kwa Kuala Lumpur, Dubai, Riyadh na Mnama nchini Bahrein,” amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori amesema matokeo hayo yanatoa chachu kwa Benki kuendeleza ubunifu, kuimarisha utawala bora na kupanua fursa za fedha shirikishi na zenye maadili katika soko.
“Tunafarijika sana kuona imani kubwa kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo washirika wetu kama vile British International Investment (BII),” amesema Profesa Neema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Sharia ya Al Barakah, Abdul Van Mohammed amesema juhudi za Serikali kuanzisha sheria maalumu ya huduma za fedha za Kiislamu zitakuwa na mchango mkubwa wa kuimarisha huduma na uwekezaji halal nchini kwani hatua hii itafungua fursa mpya kwa Tanzania kushirikiana na masoko yenye ukwasi mkubwa zikiwamo nchi za Kiarabu za Ghuba (GCC).

Hafla ya kutangaza matokeo na kuorodheshwa kwa hatifungani ya CRDB Al Barakah Sukuk ilihitimishwa kwa kupigwa kwa kengele ikiahiria kuorodheshwa kwake katika Soko la Hisa la Dar es Salaam. Kuorodheshwa huku kunawawezesha wawekezaji kujihusisha na miamala katika mazingira yaliyodhibitiwa, yenye uwazi na fursa endelevu za uwekezaji wa kiadili.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021, CRDB Al Barakah imeendelea kukua kwa kasi, ikihudumia zaidi ya wateja 400,000, ikiwa na amana zaidi ya Shilingi bilioni 350, na kutoa uwezeshaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 287 katika miradi inayozingatia misingi ya Sharia.
Mafanikio ya hatifungni ya CRDB Al Barakah Sukuk yanaashiria mwanzo wa zama mpya za fedha za Kiislamu nchini Tanzania na kuonyesha uwezo wa taifa kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka ndani na nje ya nchi.


