Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

VIONGOZI wa Serikali za Mitaa wametajwa kuwa watu muhimu katika kusimamia miundo mbinu ya umeme kutokana na ukaribu wao na wananchi na nafasi yao katika kuratibu taarifa za huduma katika maeneo yao.

Akizungumza leo Novemba 20, 2025 wakati akifungua mafunzo maalumu kwa viongozi wa kata na mitaa katika Wilaya ya Ilala, Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo, amesema serikali inatambua na kuthamini ushirikiano unaoendelea kati ya viongozi hao na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika kuhakikisha huduma za umeme zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa ufanisi.

Mpogolo amesema viongozi wa mitaa wana wajibu wa kuwasaidia wananchi kufahamu hatua sahihi za kuripoti hitilafu za umeme kupitia mfumo mpya wa Nihudumie, unaotoa huduma kwa haraka na bila gharama.

“Viongozi ni watu muhimu katika kusimamia ulinzi wa miundombinu ya umeme, ikiwemo nguzo na nyaya, hasa katika maeneo ya mijini ambayo yanakabiliwa na uharibifu wa mara kwa mara kutokana na shughuli za ujenzi.

“Uharibifu mwingine unachangiwa na watu wanaounganisha umeme kiholela, jambo linalosababisha madhara kwa jamii na kuilazimu TANESCO kubeba lawama zisizostahili,” amesema DC Mpogolo.

Amesema umeme ni miongoni mwa changamoto zinazolalamikiwa hivyo ni muhimu wao kushirikiana kwa karibu na TANESCO katika kutatua matatizo hayo na kuboresha usambazaji wa nishati.

Mpogolo pia ametoa rai kwa viongozi wa wilaya na TANESCO kuendeleza mafunzo kama hayo katika maeneo mengine ya Jiji ili kuongeza uelewa na kuimarisha mahusiano baina ya shirika hilo na viongozi wa maeneo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja TANESCO, Irene Gowele, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Lazaro Twange, amesema TANESCO imeanzisha mkakati wa kuboresha mawasiliano na viongozi wa mitaa ili kuharakisha utoaji huduma na utekelezaji wa miradi.

Amesema kupitia mafunzo hayo, viongozi wataelezwa miradi ya kimkakati inayoendelea katika maeneo yao na jinsi wanavyoweza kuwa kiungo muhimu kati ya wananchi na TANESCO.

“Viongozi hawa ndio macho na masikio ya serikali katika maeneo yao. Tukifanya kazi nao kwa karibu, tunawafikia wananchi haraka na kwa uhakika zaidi,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Abbas Mwegamno, ameishukuru TANESCO kwa kuwashirikisha viongozi hao na kuwapa uelewa kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme, hatua aliyosema inaongeza uwezo wa kupeleka taarifa sahihi kwa wananchi kama inavyoelekezwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema kuonyesha maendeleo ya miradi mikubwa, ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) ambao umeelezwa kukamilika kwa asilimia 100 na kuzalisha megawati 115,000, kumetoa matumaini mapya kuhusu upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini.

Aidha, amesisitiza kuwa viongozi wa mitaa wako tayari kushirikiana kikamilifu na serikali pamoja na TANESCO katika kuwafikishia wananchi elimu, taarifa na huduma za umeme.