Na. Asia Singano, WF, Dar Es Salaam.
Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya Vyuo Vikuu na vya Kati na kuongeza idadi ya vyuo hivyo katika mikoa yote ili wananchi wapate fursa zaidi ya kujiendeleza kimasomo na kupata elimu ya juu.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), Naibu katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, katika Mahafali ya Hamsini na Moja ya Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM), yaliyofanyika katika Ukumbi wa The Dimond Jubilee Hall, alisema Serikali imetekeleza na inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali kuboresha elimu ili kukuza uchumi.

‘’Ukuaji huu unajidhihirisha kwenye maeneo mbalimbali ya sekta, hususani; uwepo wa mradi wa SHULE BORA, mradi wa kuendeleza elimu ya Ualimu (TESP), mradi wa kuimarisha elimu ya Sekondari (SEQUIP), Mradi wa Uwezeshaji kupitia Ujuzi (ESP), mradi wa programu ya kutekeleza elimu kwa matokeo (EP4R), mradi wa kujenga ujuzi na ushirikiano Afrika Mashariki (EASTRIP), Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) pamoja na miradi mingine’’ alisema Bw. Mwandumbya.
Bw. Mwandumbya alikipongeza chuo cha IFM kwa kutoa elimu bora kwa mfumo unaoendana na mazingira ya sasa kutokana na ukuaji wa teknolojia ili kuwafikia wanafunzi wengi kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.
‘’Naendelea kuwapongeza baada ya kusikia kuwa mnakaribia kuanza kutoa mafunzo kwa njia inayounganisha teknolojia ya ana kwa ana (Blended mode), na hasa baada ya kukamilisha maboresho ya mitaala yenu kwa kuwa Elimu ya sasa inahitaji mifumo bora ya TEHAMA ili kusaidia kufikia watu zaidi’’ alisema Bw. Mwandumbya.
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi, Mkuu wa Chuo Cha IFM, Profesa. Josephat Lotto, alisema katika kuhakikisha Chuo hicho kinaendana na mazingira na mahitaji ya sasa, chuo kimeanzisha kozi mbalimbali ili kuboresha ufanisi zaidi.

‘’Chuo kimeazisha kozi mahususi ikiwemo kozi ya usalama mtandaoni, kozi inayohusisha uchanganuzi wa data, na kozi katika eneo la Uhasibu na Teknolojia, kwa ajili ya kujibu changamoto za kisekta’’ alisema Prof. Lotto.
Profesa Lotto, alitumia nafasi hiyo kuwatangazia wanafunzi waliyohitimu shahada mbalimbali kuwa chuo kinatarajia kuanzisha shahada za uzamili katika kozi mbalimbali hivyo wahitimu hao wanakaribishwa kuendelea na masomo katika chuo hicho mara tu baada ya kozi hizo kuanza.

