*Asema lengo ni kuhakikisha uchumi wa Taifa unaendelea kukua
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesisitiza kuwa Tanzania haiwezi kujenga uchumi wa kati endapo baadhi ya watendaji hawatekelezi wajibu wao ipasavyo.
Ameyasema hayo Novemba 21, 2025 wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Bombadia, Singida, ambapo amewataka watumishi kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi ili kufikia malengo ya Serikali ya kukuza uchumi.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali haitavumilia watumishi wa umma wanaowasumbua wananchi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa makusudi.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa watumishi wote wa umma wanapaswa kuwahudumia wananchi kwa weledi, kusikiliza kero zao, kuweka kumbukumbu sahihi na kufanyia kazi changamoto wanazowasilisha.
“Haiwezekani mwananchi anaenda ofisini kutafuta ufumbuzi lakini anazungushwa. Huu siyo uelekeo wa Serikali ya Rais Dkt. Samia,” amesema.
Dkt. Mwigulu amewataka watendaji wa Serikali kufuata wananchi katika maeneo yao, kuwasikiliza na kutatua kero zao bila kusubiri malalamiko kufika hadi ngazi za juu. “Mkitaka wananchi wasibebe mabango, wafikieni na wasikilizeni changamoto zao,” amesema.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu pia ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ya kuendelea kuhakikisha nchi inabaki salama, yenye mshikamano na inayolindwa na Watanzania wote.
“Tuepuke vitendo vinavyoweza kuivunjia heshima Tanzania, vijana endeleeni kuilinda na kuipenda nchi hii. Tanzania ni mali ya Watanzania, si ya viongozi wala vyama vya siasa. Tuilinde na tusikubali kudanganywa kufanya vitendo visivyofaa,” amesema.
Aidha, Dkt. Mwigulu amesisitiza uwezo mkubwa wa Tanzania uliopewa na Mungu kwa kuwa na rasilimali adimu kama madini, gesi na utajiri mwingine ambao umeifanya Tanzania kuwa na fursa nyingi. “Wananchi msikubali mgawanyiko unaochochewa na wale wanaokerwa na mafanikio ya nchi. “Twendeni tutatue kasoro sisi wenyewe; tuache nchi ikiwa salama,” ameongeza.
Pia, Waziri Mkuu amewakumbusha vijana kuhusu fursa zilizopo kupitia Wizara mpya ya Vijana iliyoanzishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema wizara hiyo imelenga kuimarisha usimamizi wa masuala yote yanayowahusu vijana nchini.

