Na Mwandishi Wetu

IMEELEZWA kuwa Mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia umeendelea kuleta matokeo chanya katika maeneo ya masoko kwa wafanyabiashara wa soko la Samaki Feri kubadili mifumo yao ya kupikia kutoka kwenye kuni na mkaa na kuhamia kwenye matumizi ya gesi, hali ambayo imeimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, pamoja na kupunguza magonjwa katika mfumo wa upumuaji yanayotokana na moshi, kulinda misitu, na kuongeza fursa za kiuchumi kupitia uwekezaji katika teknolojia na vifaa vya nishati safi vya kupikia.

Hayo yalibainishwa juzi Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Nishati safi ya kupikia Wizara ya Nishati Bw. Ngereja Mgejwa wakati akizungumza na wananchi katika kipindi cha Jambo Tanzania kikiwa mubashara maeneo ya Soko la samaki Feri, lengo likiwa ni kuhamasisha jamii kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Tunapotekeleza mkakati mkubwa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia tunatekeleza pia makubaliano ya kimataifa yanayolenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa chanzo kikuu cha uchafuzi wa mazingira na athari kwa afya za watumiaji, ambapo dhamira ya Serikali ni asilimia 80 ya wananchi watumie nishati safi ya kupikia ifikapo 2034” alihimiza Mgejwa.

Aidha alifafanua kuwa uhamasishaji unaoendelea umewasaidia wafanyabiashara kutambua faida za kutumia nishati safi ya kupikia ambazo ni salama, rahisi na fanisi kwa uchumi huku akiwapongeza wafanyabiashara wa soko la Samaki Feri kwa kuendelea kuunga mkono Juhudi za Serikali na kuhama kutoka kwenye kuni na kutumia nishati safi ya gesi kwa ajili ya kupikia.

Kwa upande wake Mhandisi Mwandamizi wa utafiti kutoka Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Bi. Catherine Mwegoha ameeleza kuwa Mkakati wa Taifa wa Nishati safi ya kupikia ni dhana muhimu ya kufanikisha malengo ya Taifa ya kuhakikisha usalama uendelevu na urahisi wa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwani Serikali imeendelea na ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji, usarishaji na usambazaji wa umeme katika mikoa yote kwa upande wa Tanzania Bara ambapo lengo ni kufikia miji na vijiji vyote nchini pamoja na kuimarisha kuwepo kwa umeme katika gridi ya Taifa, ikiwa ni Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2021/22 – 2025/26 lengo likiwa ni kukisha umeme kwa asilimia 85 ya Watanzania nchini.

“Sisi kama TANESCO tumeendelea kutoa elimu juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia hususani nishati ya umeme kwani ni salama na nafuu kwa watumiaji hususani kwa kutumia majiko kama “Pressure Cooker” na “Induction cooker” (Jiko Janja ) kwani majiko haya yamefanyiwa utafiti na hupika vyakula vya asili kama vile ugali maharage makande na ndizi kwa kutumia umeme kidogo ukilinganisha na majiko mengine” alisisitiza Mwegoha.

Naye Mhandisi Nishati safi ya kupikia Wizara ya Nishati Bw. Benezeth Kabunduguru ameeleza kuwa Mkakati wa mawasiliano umetokana na Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na lengo lake ni kutoa elimu na kuwawezesha watanzania kupata taarifa sahihi juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, elimu hii wanaipata kupitia njia mbalimbali ikiwemo redio, televisheni, mitandao ya kijamii na maonyesho ya wazi.