Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshiriki Mkutano wa 47 wa Baraza la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Afrika Mashariki (SCTIFI) na Mkutano wa Dharura Pili wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wanaosimamia Masuala ya Fedha na Uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliyofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 25 Novemba 2025 jijini Nairobi, Kenya. 

Mikutano hiyo pamoja na masuala mengine imepokea na kujadili taarifa za kamati zinazosimamia masuala ya Biashara, forodha, uwekezaji, kamati ya viwango na mamlaka ya ushindani ya Afrika Mashariki. 

Vilevile, mawaziri hao wamepokea na kujadili na orodha ya ada, tozo na ushuru usiozingatia usawa, unaotozwa na nchi wanachama kinyume na matakwa ya Ibara ya 10 na ya 15 ya Itifaki ya Umoja wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mikutano hiyo miwili muhimu umejumuisha Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango – Zanzibar, Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango- Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil.  

Mkutano huo umehudhuriwa na nchi zote nane (8) wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.