Na. OR -MV Songwe
Vijana mkoani Songwe wamepongeza uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuunda wizara maalum itakayoshughulika na agenda za maendelo ya vijana na kusema hatua hiyo itasaidia jitihada za kuongeza fursa za kiuchumia na upatikanaji ajira.
Wakizingumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Joel Nanauka akiwa ziarani wilaya ya Songwe leo (26 Novemba 2025) vvijana wajasiliamali katika soko la Mkwajuni, waendesha boda boda na waachimbaji wadogo wa madini kijiji cha Saza walisema wana imani kuwa wizara hii itatumika kuwafikia na kuwasikiliza .
Mwenyekiti wa vijana waendesha bodaboda Mkwajuni wilaya Songwe, Hamisi Jairi alisema kitendo cha kutembelewa na kusikilizwa na Waziri kisiwe cha Mwisho bali changamoto zao zipatiwe ufumbuzi haraka.

Jairi aliomba serikali kupitia Wizara ya Vijana kutatua changamoto ya upatikanaji vyuo vya mafunzo ya udereva ili vijana waweze kupata ujuzi na hatimaye wapate leseni za kuendesha vyombo vya moto ambapo pia aliomba vijana wasaidiwe kuunganishwa kwenye vikundi na kupatiwa Bima za Afya ili wawe na uhakika wa matibabu.
Kwa upande wake Zacharia Matogoro mjasiliamali katika soko la Mkwajuni ambaye pia ni mhitimu wa shahada ya Lugha toka Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka 2022 alisema changamoto kubwa inayomkabili ni ukosefu wa mtaji kuweza kukuza biashara yake ya duka pamoja na miundombinu isiyoridhisha ya soko.
Nikiwezeshwa mkopo wa kati ya shilingi milioni 3 au 4 naweza ongeza mtaji kwa biashara yangu na kuwa na uhakika wa kurejesha mkopo huo alisema Matogoro.
Naye Mwenyekiti wa wachimbaji Wadogo madini Kijiji cha Saza Shadrack Mwakyalyabwe alisema ni wakati sasa Serikali ikachukua hatua za kusaidia vijana wajasiliamali wenye viwanda kupata mitaji ili waweze kuajili vijana wenzao hatua itakayosaidia kukuza uchumi na kuondoa changamoto za ajira.

Kufuatia mazungumzo yake na vijana hao, Waziri Nanauka ameagiza halmashauri zote nchini kuandaa mazingira wezeshi ili fedha za uwezeshaji wa vijana zitakazotolewa ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ziweze kuwafikia bila vikwazo hatua itakayochangia vijana wengi nchini kupata uhakika wa mitaji .
Waziri Nanauka aliwahakikishia vijana kuwa Rais Samia ana maono ya kutaka kuona vijana wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa kupitia shughuli za uzalishaji mali hivyo kuamua kuunda wizara maalum.
Aidha, Nanauka akiendelea na ziara mkoani Songwe amewaeleza vijana falsafa ambayo katika kipindi cha uongozi wake ndani ya Wizara ya Vijana ataisimamia kwa Kauli mbiu isemayo Vijana Tuyajenge, Tanzania ni Yetu” ambayo ina maanisha kuwa hatma ya Tanzania iko mikononi mwa vijana na hivyo kuhitaji vijana wote washikamane na Serikali kutafuta suluhisho la changamoto zao.
Amesema falsafa ya kwanza, kasi katika kuhudumia vijana ambapo Nanauka amewataka viongozi na watendaji wote katika ngazi ya wizara, mikoa na halmashauri kutatua na kushughulikia masuala ya vijana kwa kasi ikiwemo kero na changamoto.
Falsafa ya pili ni kuhakikisha vijana wanasikilizwa na kufuatwa mahali walipo.
“Katika kutekeleza hili ndio maana hata mimi Waziri nayeshughulikia masuala ya vijana nimeamua kufanya ziara mikoani kukutana na kuzungumza na vijana na nimeagiza watendaji wasikae ofisini bali wawafuate vijana kwenye maeneo yao na kuwasilikiza,” amesema
Falsafa ya tatu ni kuwekeza katika matumizi ya teknolojia kwa kuanzisha mfumo maalum wa kuwafikia vijana nchini hatua itakayosaidia kuratibu masuala ya vijana ikiwemo kupata mawazo yao na kutoa majawabu kwa changamoto zinazowakaribi.
Vile vile, Waziri Nanauka aliongeza kuwa mfumo huo utakaonzishwa (Vijana App) umatumika kama jukwaa la kupeana taarifa na mrejesho juu ya masuala muhimu ya Taifa.
“Kauli mbiu hii inatutaka sisi vijana tukae chini tujadiliane ili kwenye tatizo tutafute suluhu na kisha tufanyie kazi ili amani ya nchi yetu iendelee kudumu na vijana watumie rasilimali za nchi kujiletea maendeleo “alisisitiza Waziri Nanauka.
Waziri Nanauka yuko katika ziara ya kukutana na kuzungumza na vijana katika nchini ambapo leo amehitimisha katika mkoa wa Songwe baada ya kutembelea wilaya za Momba, Mbozi na Songwe. Kituo kinachofuata ni mkoa wa Mbeya.


