Mashindano ya Riadha ya Wanawake Ladies First 2025 yanatarajiwa kufanyika Novemba 29 na 30 2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, yakihusisha wanariadha 155 kutoka mikoa 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Mashindano hayo yataongozwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano la Kimataifa la Japan (JICA) pamoja na Shirikisho la Riadha Tanzania (AT). Kabla ya mashindano kuanza, semina maalum kwa wanariadha na waamuzi itafanyika tarehe 28 Novemba 2025 kama sehemu ya maandalizi ya kitaaluma kwa washiriki.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, leo Novemba 26, 2025 Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Bi. Neema Msitha, alisema mashindano hayo ni sehemu ya juhudi endelevu za kuongeza ushiriki wa wanawake katika michezo nchini. Alisema licha ya hatua mbalimbali kuchukuliwa, bado ushiriki wa wanawake uko chini ukilinganisha na wanaume, hivyo “Ladies First” ni jukwaa mahsusi la kuibua na kukuza vipaji vya watoto wa kike.

“Serikali kupitia BMT na wadau wetu kama JICA, tumejikita katika kuongeza fursa na kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika michezo. Mashindano haya yamekuwa chachu ya kuzalisha vipaji vipya ambavyo vinaweza kuiwakilisha nchi kimataifa,” alisema Bi. Msitha.

Aliongeza kuwa pamoja na mashindano, kutakuwa na mafunzo ya matumizi ya taulo za kike, elimu ya nidhamu ya matumizi ya fedha, na upimaji wa afya kwa washiriki, hatua ambayo inalenga kuwaandaa wanariadha kuwa na ustawi wa maisha ndani na nje ya mchezo.

Mashindano yatashuhudia washiriki wakichuana katika mbio za M100, M200, M400, M800, M1500, M5000, 4x100m kupokezana vijiti, pamoja na kurusha mkuki (Javelin). Ufunguzi rasmi unatarajiwa kufanyika Novemba 29, ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri mwenye dhamana ya Michezo, Mheshimiwa Prof. Palamagamba Aidan Mwaluko Kabudi (Mb). Tukio hilo litahudhuriwa pia na viongozi kutoka Japani, JICA, Shirikisho la Riadha Tanzania na viongozi mbalimbali wa wizara.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (AT), Rogath Steven, aliipongeza BMT na JICA kwa kuendelea kuandaa mashindano hayo, akisema yamechangia pakubwa katika kuendeleza kizazi kipya cha wanariadha wa kike nchini.

“Kupitia Ladies First tumeshuhudia vipaji vinavyoibuka na kufanya vizuri katika mashindano ya ndani na nje ya nchi. Ni muhimu kwa mikoa kuendelea kuwaunga mkono wanariadha wake ili tuendelee kujenga msingi imara wa riadha ya wanawake,” alisema Rogath Steven.

Naye mwanariadha mkongwe Jumaa Ikangaa, ambaye ni mwasisi wa mashindano haya kwa kushirikiana na Serikali ya Japani kupitia JICA, alieleza kufurahishwa na jinsi mashindano haya yamekua tangu kuanzishwa mwaka 2017.

“Tulianzisha mashindano haya kwa lengo la kumsaidia mtoto wa kike kupata nafasi ya kujiamini na kuonyesha uwezo wake kwenye riadha. Leo hii tunaona mabadiliko makubwa, vipaji vipya vinaibuka kila mwaka. Huu ni wakati wa wasichana kuendelea kuthibitisha uwezo wao,” alisema Ikangaa.

Katika ufunguzi wa mashindano, kutakuwa pia na mazoezi ya viungo pamoja na mbio za “jogging” zitakazohusisha zaidi ya wakimbiaji 2,000 kutoka Wilaya ya Temeke.

BMT imetoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo, hatua ambayo itachochea hamasa na kuongeza ari kwa wanariadha kupata motisha ya kufanya vizuri zaidi.

Mashindano ya Ladies First 2025 yanatarajiwa kuwa chachu muhimu ya kuimarisha ushiriki wa wanawake katika riadha na kuendeleza historia ya taifa katika mchezo huo.