Na Mwandishi Wetu

Wakulima wa zao la korosho Wilayani Tunduru,wametakiwa kutumia fedha wanazopata kwenye mauzo ya korosho kufanya maandalizi ya msimu ujao,kuboresha makazi yao na kufanya maandalizi ya watoto wao wanaotakiwa kwenda shule katika muhula wa masomo 2026.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Denis Masanja ametoa agizo hilo jana,alipkuwa akizungumza na wakulima na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) baada ya kufanyika kwa mnada wa tatu wa zao hilo katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya mjini Tunduru.

“msimu wa korosho kwa msimu 2025/2026 unaendelea hivi sasa, kwa hiyo ni muhimu sana viongozi wetu wa Amcos kuwakumbusha wakulima kuweka akiba ya fedha kwa ajili ya mahitaji muhimu ikiwemo kununua pembejeo kwa ajili ya msimu ujao”alisema Masanja.

Masanja,amewakumbusha wakulima hao kuhakikisha wanatumia fedha kwa kuboresha makazi yao na maandalizi ya watoto wanaotakiwa kuanza na wale watakaoendelea na masomo badala ya kutumia kwenye anasa.

Masanja alisema,sio vema wakulima kutumia fedha wanazopata kucheza unyago huku wakisahau mahitaji muhimu ya familia na kuwasisitiza kuweka fedha benki badala ya kuhifadhi kwenye magodoro ili kuepuka kuibiwa.

Amewataka wakulima Wilayani Tunduru, kuzingatia na kufuata maelekezo ya wataalam wa kilimo wa BBT Korosho na maafisa ugani wa Halmashauri ya Wilaya ili waweze kuzalisha korosho bora zitakazokubalika kwenye minada inayoendeshwa na Soko la Bidhaa Tanzania(TMX)kwa kushirikiana na Chama kikuu cha Ushirika Wilayani humo(TAMCU).

Amewapongeza wakulima kwa kufanikiwa kuzalisha korosho bora ambazo katika mnada huo zimeuzwa kwa daraja la kwanza, na amewataka viongozi wa Chama kikuu cha Ushirika kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao kulingana na korosho wanazopeleka kwenye maghala huku taasisi za fedha akizitaka kulipa wakulima kwa wakati.

Kwa upande wake Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania Tawi la Tunduru Shauri Mokiwa,amewataka wakulima wa zao hilo kuandaa mashamba kwa ajili ya kupanda miche mipya ya mikorosho inayozaa haraka na kutoa mavuno mengi.

Mokiwa amesema,wakulima wanapaswa kuandaa mashamba yao mapema kwani hakuna mkulima atakayepewa miche au pembejeo kabla shamba lake halijakaguliwa na wataalam wa kilimo kwani malengo ya Serikali ni kuongeza uzalishaji wa korosho.

Mokiwa, amewashauri wakulima kuanza kupanda mazao mengine kwenye mashamba ya korosho ili kuhifadhi unyevu unaosaidia kustawisha miti ya korosho.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tamcu Mussa Manjaule amesema,watahakikisha wanalipa fedha za wakulima kwa wakati na kuwasisitiza wale wenye korosho majumbani kuhakikisha wapeleke kwenye maghala kwa ajili ya kuuzwa ili kuepusha korosho kuharibika kwa kuwa mvua zimeanza kunyesha katika maeneo mbalimbali.

Amewakumbusha kuwa,ni vema korosho zilizoko majumbani zianikwe vizuri ili kuepuka korosho kuwa na unyevu usiohitajika sokoni unaoweza kusababisha hasara kubwa kwa mkulima. mwenyewe.

Katika mnada wa tatu jumla ya kilo 9,560,021 zimeuzwa huku bei wastani ikiwa Sh.2,512 kwa kilo moja ambapo wakulima walikubali kuuza korosho zao zilizoingizwa kwenye mnada huo.

Hata hivyo,mkulima wa korosho Said Hamad,amelalamikia bei huku akisema haikuwa nzuri na kuiomna Serikali ijitahidi kuwabana wanunuzi ili waongeze bei kwenye zao hilo kutokana na uzalishaji wake kutumia gharama kubwa.

“Naishukuru Serikali kupitia Chama chetu Kikuu cha Ushirika kusimamia malipo yetu ambayo hadi sasa yanakwenda vizuri sana,lakini tunaiomba Serikali isimamie kwenye bei kwani sio nzuri na inatukatisha tamaa,mchakato wa uzalishaji wa korosho ni mgumu sana”alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Denis Masanja,akizungumza na wakulima na viongozi wa vyama vya Ushirika(Amcos) hawapo pichani,wakati wa mnada wa tatu wa zao la korosho uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Tunduru,kushoto Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tamcu Mussa Manjaule.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma(TAMCU) akitangaza bei ya zao la korosho kwenye mnada wa tatu uliofanyika jana katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Tunduru ambapo korosho iliuzwa kwa bei ya Sh2,512 kwa kilo moja,kushoto Mkuu wa Wilaya hiyo Denis Masanja.
Baadhi ya wawakilishi wa Taasisi za fedha Wilayani Tunduru,wakifuatilia mnada wa tatu wa zao la korosho uliofanyika jana katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ambapo bei ilikuwa Sh.2,512 kwa kilo moja.