Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WAZIRI wa Katiba na Sheria Dk Juma Honlmera amefurahishwa na mpango wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kuendelea kuwajengea uwezo wajumbe wa Bodi za Wadhamini kutoka taasisi mbalimbali ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza katika kuziendesha taasisi zao.

“Napenda pia kuchukua fursa hii kuishukuru RITA kwa kunialika ili kufungua Mkutano huu muhimu sana wa wajumbe wa bodi za wadhamini zilizopo mikoa ya Dodoma, Morogoro, Singida, Iringa na Manyara kwa ajili ya kuwajengea uwezo kusimamia taasisi zao,” amesema.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera (wapili kushoto) akisalimiana na baadhi ya viongozi mala baada ya kuwasili katika mkutano wa wajumbe wa Bodi za Wadhamini uliofanyika jijini Dodoma wenye kaulimbiu isemayo “Uwajibikaji wa Bodi za Wadhamini kwa Ulinzi wa Mali za Taasisi na Maendeleo ya Jamii” wakwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rosemary S. Senyamule, watatu kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya RITA Dr. Amina Msengwa , na wapili kulia ni Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi.

Mkutano huo ulifanyika jana katika ukumbi wa Mikutano wa Saint Gasper mkoani Dodoma chini ya kaulimbiu “UWAJIBIKAJI WA BODI ZA WADHAMINI KWA ULINZI WA MALI ZA TAASISI NA MAENDELEO YA JAMII” ulilenga moja kwa moja kuimarisha misingi ya utawala bora, uwajibikaji na uadilifu katika usimamizi na utunzaji wa mali za taasisi mbalimbali nchini.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Dkt. Homera amesema kuwa Bodi za Wadhamini ni nguzo muhimu katika ustawi wa taasisi zisizo za kiserikali, taasisi za kidini, michezo, na taasisi nyingi zinazotoa huduma mbalimbali kwa jamii.

Hivyo, ameongeza kuwa mkutano huo ni muhimu kwani utawezesha kupunguza au kumaliza kabisa changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya bodi za wadhamini na hivyo kuziathiri taasisi wanazozisimamia.

Hata hivyo, Waziri Homeya amesema kuwa mbali na mafanikio yaliyopatikaa,bado ipo changamoto ya baadhi ya bodi za wadhamini kutotimiza majukumu yao kikamilifu kwa kutumia mali za taasisi kwa maslahi binafsi, kufanya ubadhirifu wa mali na fedha, kujimilikisha mali kinyume cha utaratibu, Bodi za Wadhamini kukaa madarakani zaidi ya muda ulioainishwa katika Katiba hivyo kusababisha migogoro na uvunjifu wa amani.

Pamoja na changamoto hizo, ameipongeza RITA kwa hatua mbalimbali inazochukua kwa lengo la kutatua na kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika Bodi za Wadhamini.

Pia ameisifu RITa kwa mageuzi mbalimbali ya kiutendaji, ikiwemo kuwezesha huduma za Bodi za Wadhamini kupatikana kidijitali kupitia mfumo wa eRITA.

“Hakika haya ni mageuzi makubwa yanayoendana na wakati tuliopo ambao bila matumizi ya mifumo ya kidijitali taasisi haiwezi kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wadau wake,” amesema.

Amesema kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki za kisheria na kiutawala zitachukuliwa kwa wale wote wanaokiuka misingi ya Sheria katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Taasisi zake imedhamiria kuhakikisha kila taasisi inasimamiwa na Bodi ya Wadhamini yenye uadilifu, ujuzi na uwezo wa kuhakikisha mali na rasilimali za taasisi zinafanya kazi kwa manufaa ywanachama.

Pamoja na mambp mengine, imeagiza RITA kufanya mapitio ya sheria na kanuni za usajili wa bodi za wadhamini ili ziendane na mahitaji ya sasa.

“Mapendekezo yote ya maboresho yanayohitajika yawasilishwe katika Wizara yangu mapema ili michakato ya maboresho ianze,” amesema,

Maagizo mengine aliyoyatoa ni pamoja na kukamilisha maboresho ya mfumo wa eRITA ili uweze kuwa rafiki kwa watumiaji katika usajili, uwasilishaji na ufuatiliaji wa taarifa.

Pia ameiagiza RITA kuhakikisha kuwa maboresho hayo yanabeba mipango ya mbele ya taasisi kuhusu eneo la usajili, udhibiti na usimamizi wa Bodi za Wadhamini.

Lakini pia ameiagiza RITA iongeze wigo wa huduma za “Mobile Clinics” katika maeneo yote ili kusogeza huduma karibu na wadau.

Wadau na wajumbe wa Bodi za Wadhamini kutoka mikoa ya Dodoma, Morogoro, Singida, Iringa na Manyara, wakifuatilia mkutano uliolenga Uwajibikaji wa Bodi za Wadhamini kwa Ulinzi wa Mali za Taasisi na Maendeleo ya Jamii uliofanyika jana jijini Dodoma. Ulizinduliwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera.

Pia ameitaka RITA iongeze kasi ya elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari hususan kunapokuwa ma mabadiliko katika mifumo ya utoaji huduma.

Pia amewataka wajumbe wa Bodi za Wadhamini kuzingatia sheria, kanuni na katiba za taasisi zao katika utekelezaji wa majukumu yao na kuhakikisha mali na rasilimali za taasisi zinalindwa na kutumiwa kwa manufaa ya wanachama na si vinginevyo.

Pia wahakikishe wanawasilisha taarifa kwa wakati kwa RITA kupitia mfumo wa kidijitali wa eRITA na kuwataka kuepuka migogoro ya kiuongozi kwa kufuata utaratibu katika kufanya mabadiliko ya Wajumbe.

Awali, wakati akimkaribisha Waziri, Mtendaji Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Bw. Frank Kanyusi ametaja majukumu ya msingi ya wajumbe wa Bodi za Wadhamini na kueleza kwamba wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Bodi za Wadhamini Sura ya 318 toleo la 2002 katika kutekeleza majukumu yao ya kusimamia taasisi zao, ikiwemo kuhakikisha mali za taasisi hizo zinalindwa na kutumika kwa matumizi sahihi.

Aidha, Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA Bw. Frank Kanyusi ameweka wazi kwamba Wadhamini wamepewa mamlaka na kuaminiwa kusimamia mali za Taasisi kwa faida ya wanachama au wanufaika kulingana na madhumuni ya kuanzishwa taasisi husika kama yalivyoainishwa katika katiba.

Amesema kuwa taasisi hiyo inakusudia kuanzisha huduma za “mobile Clinics” kwa lengo la kutoa ushauri, kutatua changamoto papo kwa papo, na kusogeza huduma karibu na wadau.

Bw. Kanyusi amesema kuwa Usajili wa Bodi ya Wadhamini ni hatua muhimu kwani inaipa taasisi na utu wa kisheria wa kumiliki mali, kuingia mikataba kwa niaba ya Taasisi, kushitaki au kushitakiwa niaba ya Taasisi.

Ameongeza kuwa Utaratibu huu unaongozwa na Sheria ya Usajili wa Bodi za Wadhamini Sura ya 318 toleo la 2002. (The trustees’ Incorporation Act CAP 318 R.E. 2002).

Amezitaja taasisi zinazotakiwa kuwa na Bodi ya Wadhamini ni pamoja na vyama vya siasa, taasisi na madhehebu ya kidini, vyama / vilabu vya michezo mfano: mpira wa miguu, mpira wa mikono, mpira wa vikapu nk, Taasisi binafsi za kijamii zinazomiliki mali, vyama vya Kiuchumi na vyama vya kitaaluma.

“ Mheshimiwa mgeni rasmi, Sheria niliyoitaja hapo juu inanipa Mamlaka mimi Kabidhi Wasii Mkuu (Administartor General) kuwa Msajili Mkuu nikiwa na jukumu la kusimamia na kuratibu Usajili na utendaji kazi wa Bodi za Wadhamini,”.

“Mpaka sasa wakala umefanikiwa kusajili jumla ya bodi za wadhamini 5211 na kati ya hizo, bodi 2876 ni za Taasisi za Kijamii, Bodi 2161 ni Taasisi za kidini, bodi 19 ni zaVyama vya Siasa , Bodi 24 ni za Vyama vya Michezo na bodi 150 ni Taasisi za Kifamilia,”.

Bw. Kanyusi amesema Pamoja na sheria kuainisha majukumu na wajibu wa wajumbe wa Bodi za Wadhamini, bado zipo changamoto kwa baadhi ya bodi kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Amezitaja baadhi ya Changamoto hizo kuwa ni pamoja na:

Usimamizi usioridhisha wa mali na rasilimali za taasisi, uelewa mdogo wa sheria, kanuni na wajibu wa wadhamini,mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi bila kufata taratibu, migogoro ya kiuongozi ndani ya bodi za wadhamini, uwasilishaji hafifu wa taarifa za bodi kwa RITA na

kutotumia kikamilifu mfumo ya kidijitali wa eRITA.

Aidha, amesema kuwa changamoto zilizoainishwa hapo juu zinatoa taswira kwamba uwezo wa baadhi ya Bodi za Wadhamini unahitaji kuimarishwa ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza ambayo hatimaye yanaweza kuathiri ustawi na utendaji wa taasisi na umma kwa ujumla.

Amesisitiza kuwa RITA inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kukabiliana na changamoto zilizoainishwa hapo juu ikiwa pamoja na kuimarisha mifumo ya kidijitali—hususan mfumo wa eRITA—ili kurahisisha utunzaji na uwasilishaji wa taarifa za bodi.

Pia RITA itaendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Wadhamini ili kuongeza uelewa wa majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Pia ameongeza kuwa RITA inakusudia kuanzisha huduma za “mobile Clinics” kwa lengo la kutoa ushauri, kutatua changamoto papo kwa papo, na kusogeza huduma karibu na wadau.

RITA imebuni mfumo wa kielektroniki wa utoaji huduma kwa wadau wa eRITA ambapo huduma za Udhamini ni moja ya huduma inayopatikana kwa haraka na urahisi kupitia mfumo huo. Hivyo, Wadhamini kwa sasa wanaweza kufanya marejesho ya mwaka, kubadili taarifa za taasisi, kutuma maombi ya kumiliki ardhi na huduma nyinginezo bila kufika Ofisi za Wakala.

Wakala umefanya maboresho haya kwa lengo kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuboresha upatikanaji na utunzaji wa taarifa za Wadhamini.

Mkutano huu uliwahusu Wadau wa usajili na usimamizi wa Bodi za wadhamini ambao ni pamoja na Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Maafisa Tarafa, Mamlaka Kuu za Usimamizi wa Taasisi (supreme Authorities) pia na Wajumbe wa Bodi za Wadhamini wa Taasisi kutoka mikoa mitano ya mitano ya Dodoma, Iringa, Morogoro, Singida na Manyara.