Kwa mara ya kwanza Tanzani imeshinda tuzo kuu za uhifadhi Duniani katika hafla iliyofanyika jiji la London nchini Uingereza, usiku wa kuamkia leo Novemba 27, 2025 tuzo hiyo ni maarufu kwa jina la Tusk for Conservation in Africa.
Mshindi wa tuzo hiyo ni Bi. Rahima Njaidi, ambaye ni Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA).
Tuzo hizo zinawatambua wahifadhi wa Kiafrika, ambao wameendeleza uvumbuzi na athari kubwa katika ulinzi wa bioanuwai katika bara zima.
Tuzo hizo tangu kuanza kwake huu ni mwaka wa 13, hufanyika kila mwaka kwa ushirikiano na Meneja wa Uwekezaji wa Ninety One na wamewatunuku washindi 57 waliotangulia.
Bi. Rahima, ni mwanasheria aliyejitolea na kiongozi wa uhifadhi wa misitu, anatambulika kwa karibu miongo miwili ya kazi ya kuziwezesha jamii za vijijini kupitia Usimamizi wa Misitu yenye Msingi wa Jamii (CBFM), utawala bora na maisha endelevu.
Aidha, kupitia MJUMITA inaongoza mashirika 132 ya kijamii (CBOs) yanayofanya kazi katika vijiji 503 nchini Tanzania, vinavyotetea ulinzi wa misitu, uhifadhi wa bioanuwai, na kupata haki za ardhi za jamii.
Tuzo za Tusk Conservation huwaheshimu mashujaa wa uhifadhi wa Afrika, na kusaidia kusimulia hadithi zao kwa ulimwengu.
Tangu kuanzishwa kwao mwaka wa 2013, Tuzo hizi zimetumika kama chachu kwa wahifadhi wa mazingira bora barani Afrika na kuleta umakini mkubwa wa Kimataifa kwa kazi zao.
Walinzi hawa wa bioanuwai wamepanda juu katika nyanja zao, wakiongeza kazi zao, na kuongeza athari za uhifadhi katika bara zima.



