Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ameiagiza sekta ya mifugo kuongeza ubunifu, kufanya tafiti zenye matokeo na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo ili kuongeza ushindani kimataifa na tija kwa wafugaji.

Bashiru alitoa maagizo hayo, Novemba 27, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua viwanda vinavyozalisha mazao ya mifugo ikiwemo kiwanda cha kusindika nyama cha TANCHOICE, UNION MEAT, kiwanda cha kuzalisha vyakula vya mifugo na samaki (BACKBONE) pamoja na kiwanda cha kuzalisha chanjo (HESTER BIOSCIENCES).

Alisema sekta ya mifugo ina mchango mkubwa katika uchumi, hivyo ni muhimu wadau kutoa mawazo chanya na kushiriki kikamilifu katika kutafuta suluhisho la changamoto zilizopo.

“Kama kuna makosa, kero au changamoto zibainishwe wazi, Na kama kuna maoni ya msingi ya kutatua changamoto hizo, yatoeni ili tujenge mijadala yenye tija na mawasiliano ya kimkakati yatakayotoa matokeo chanya kwa wananchi,” alielezea Bashiru.

Alisisitiza umuhimu wa watendaji wa sekta hiyo kuendelea kutoa mawazo chanya, kufanya tafiti zenye tija na kutumia fikra bunifu zitakazochochea ubunifu katika kuboresha mazao ya mifugo na kuongeza mnyororo wa thamani.

Vilevile, Bashiru alihimiza utekelezaji wa mkakati wa kuongeza thamani ya mazao ya mifugo kwa vitendo ili kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi na wafugaji.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani, alipongeza uongozi wa mkoa wa Pwani kwa kuweka mazingira wezeshi yaliyovutia wawekezaji hao.

Alisema hatua hiyo inaendana na dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kufanya mageuzi ya uchumi kupitia sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kuongeza mnyororo wa thamani.

Akitoa taarifa ya mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, alisema uzalishaji wa mifugo umeongezeka kwa kasi kutokana na kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za ugani, maji, malisho na udhibiti wa magonjwa kupitia uogeshaji na chanjo.

Alisema kati ya mwaka 2023/2024 na 2024/2025 idadi ya mifugo imeongezeka ng’ombe kutoka 683,218 hadi 694,447,Mbuzi kutoka 273,292 hadi 279,310, Kondoo kutoka 106,122 hadi 108,596,Nguruwe kutoka 26,895 hadi 42,614,Punda kutoka 3,220 hadi 3,243 na Kuku kutoka 3,187,097 hadi 3,727,863.

Aidha, uzalishaji wa mazao ya mifugo umeongezeka kutoka mwaka 2023/2024 hadi 2024/2025 kama maziwa kutoka lita 21,023,471 hadi 21,123,448,Nyama kutoka tani 7,526 hadi 8,677, mayai kutoka trei 16,555,028 hadi 16,605,941,Ngozi (mbuzi na kondoo) kutoka vipande 105,884 hadi 107,839.

Nae Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji mkoa wa Pwani, Ngobere Msamau, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajengea mazingira wezeshi, ikiwemo ruzuku ya chanjo za mifugo na uwekezaji wa viwanda vya kusindika nyama ambavyo vimepanua soko la mifugo yao.