Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Katiba na Sheria ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma Dkt Juma Homera amesema,katika msimu wa kilimo 2025/2025 wakulima wataanza kulima zao la Kakao kama mkakati wa Wilaya hiyo kuwa na mazao mengi zaidi ya kibiashara na kiuchumi.
Waziri Homera alisema hayo jana,wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa Chama cha Mapinduz (CCM) waliojitokeza kwenye ofisi ya Chama cha Mapinduzi Wilayani Namtumbo.
Waziri Homera alisema,zao la kakao lina thamani kubwa kiuchumi kwani kilo moja ya zao hilo huuzwa kwa Sh.15,000 ambao amesisitiza kuwa, mpango huo utafanikiwa Wilaya hiyo inaweza kupiga hatua kubwa ya kiuchumi kama ilivyo wilaya nyingine za Mkoa wa Ruvuma.
“Kwa kuanzia tayari nimenunua miche 40,000 kwa fedha zangu mwenyewe kutoka Mkoani Mbeya ambayo itatolewa bure kwa wakulima hasa wale wanaofanya shughuli za kilimo kwenye vijiji vya Msisima,Magazini na Sasawala ambako kuna ardhi nzuri inayostawi zao hilo”alisema Dkt Homera.
Alisema,lengo ni kuwapunguziwa wakulima gharama kwenye shughuli zao kilimo ikiwemo mbegu na pembejeo zinauzwa kwa bei ya juu na wafanyabiashara wa mitaani.
Kuhusu zao la ufuta Dkt Homera alisema,tayari amenunua zaidi ya tani 3,000 ya mbegu za ufuta ambazo zitasambazwa kwenye vijiji mbalimbali ili kuwaondolea wakulima usumbufu wa kutafuta mbegu na kuwahamasisha kulima zao hilo lenye faida na mchango mkubwa kiuchumi.
“Kwenye utekelezaji wa mpango huu nitalipia gharama za kuandaa mashamba kwa vijana,wanawake na wazee hekari tano tano kwenye kila kijiji,wao ndiyo watachagua aina ya mazao wanayotaka kulima,naamini hatua hii itawezesha wananchi wa jimbo langu kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli za kilimo”alisema Homera.
“Nilichokipata lazima nigawane na wenzangu ndiyo maana nimeona kimbie kuja nyumbani mara moja tuongee ili yale niliyohaidi wakati wa kampeni yaanze kufanyiwa kazi”alisisitiza Dkt Homera.
Katika hatua nyingine Dkt Homera alisema,atahakikisha anasimamia kwa karibu masoko ya mazao ili wakulima wapate bei nzuri na walipwe kwa wakati baada ya kufikisha sokoni ili waweze kunufaika na jitihada wanazofanya kwenye uzalishaji.
Aliwataka wananchi wa jimbo hilo hususani vijana,kujikita kwenye kwenye kilimo kwani kina mchango mkubwa kiuchumi wa mtu mmoja mmoja,badala ya kushawishika na uzushi wa mitandaoni unaohamasisha maandamano ambayo hayana faida kwao.
Alisema,Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuchukua hatua kwa kuboresha na kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo miundombinu ya Barabara ambapo tayari imenaza ukarabati wa Daraja la Namali ambalo awali halikuwa salama kwa wananchi wanaopita eneo hilo hasa wakati wa masika.
Alisema,ukarabati hu oni miongoni mwa jitihada za Serikali kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa hasa mazao ya kilimo kutoka shambani kwenda sokoni.

