Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

Diwani Mteule wa Kata ya Tumbi, Dkt. Mawazo Nicas, ameshinda nafasi ya Ustahiki Meya wa Manispaa ya Mji Kibaha kupitia kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kupata kura 15 kati ya 19 zilizopigwa na madiwani wateule.

Katika uchaguzi huo, Aziza Mruma, Diwani wa Viti Maalum, alichaguliwa kuwa Naibu Meya baada ya kupata kura 10.

Akizungumza mara baada ya uchaguzi uliofanyika katika Ofisi ya CCM Kibaha Mjini, Dkt. Nicas aliwahakikishia wananchi wa Manispaa ya Kibaha kuwa ataongoza maendeleo kwa usawa bila kubagua kata yoyote.

Amesema amejipanga kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini pamoja na watendaji wa Manispaa hiyo ili kuwainua wananchi, hususan wale wasio na sauti.

“Nawashukuru wajumbe wa Kamati Kuu kwa kuniteua miongoni mwa majina matatu yaliyorejeshwa, nawashukuru madiwani wenzangu kwa kuniamini. Uchaguzi ulikuwa wa wazi na umefanyika kwa utulivu, .

“Hili ni deni wananchi wategemee kasi ya maendeleo na usimamizi makini wa miradi kwa maslahi ya jamii,” alielezea Dkt. Nicas.

Kwa upande wake, Aziza Mruma aliahidi kuisimamia Manispaa hiyo kuhakikisha inaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.

“Wananchi watarajie mabadiliko makubwa ya kiuchumi. Sisi tumeingia kazini, wakae mkao wa kula,” alieleza Aziza.

Katibu wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Issack Kalleiya, alifafanua wagombea waliochukua fomu ya kuwania Ustahiki Meya walikuwa wanne John Katele Diwani Mteule Kata ya Pangani, Dkt. Mawazo Nicas- Tumbi, Mashaka Mahande wa kata ya Sofu na Elinius Mapunda kata ya Mkuza.

Kamati Kuu ilirudisha majina matatu akiwemo Katele, Nicas na Mapunda ambapo katika kupiga kura, Dkt. Nicas alipata 15, akifuatiwa na Katele aliyepata 3, huku Mapunda akiambulia kura 1.

Kwa nafasi ya Naibu Meya, matokeo yalikuwa, Aziza Mruma kura 10, Ramadhani Lutambi (Mailimoja) kura 6 na Ally Simba (Misugusugu) – kura 3.

Kalleiya aliwataka madiwani kujenga umoja na kuepuka kusikiliza taarifa za upotoshaji, akisisitiza kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni za Chama na kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo kwa maslahi ya Manispaa na CCM.

Hata hivyo alibainisha, waliopitia mchakato huo wa kura za maoni wataapishwa kuwa Meya na Naibu Meya katika Baraza la Madiwani la Manispaa ya Mji Kibaha siku ya Alhamisi, Disemba 4, 2025, na ndipo watakapokuwa rasmi kuanza majukumu yao.