Rais wa Jamhuri ya Muumgano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajia kuzungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es salaam siku ya Jumanne Disemba 2 mwaka huu ambapo pia atatumia mkutano huo kulihitubia Taifa juu ya masuala mbalimbali yanayolihusu Taifa
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Mkuu wa Mkoa huo Mhe Albert Chalamila amesema hatua hiyo ya Rais Dkt Samia kuzungumza na wazee wa Mkoa huo na kulihutubia Taifa ni katika muendelezo wa dhamira yake njema ya namna bora ya kuirejesha nchi kwenye umoja wake, kuwafariji watanzania na kuimarisha demokrasia ili hatimaye kurejesha Tanzania katika hali ya kawaida ya amani, upendo na mshikamano.
RC Chalamila amewataka wana Dar es Salaam na watanzania kwa ujumla kufuatilia mkutano huo utakaofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa Mwl Julius Nyerere kuanzia saa tano asubuhi na kusisitiza kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu amekusudia kuliunganisha Taifa na kurejesha amani kama yalivyokua hapo awali
Aidha Mkuu wa Mkoa Mhe Albert Chalamila amewaasa wakazi wa jiji hilo hususani vijana kuendelea kushiriki kwenye ulinzi wa Mkoa huo na Taifa kwa ujumla ili kutunza amani kwani kupotea kwa amani hasa katika Mkoa huo ni kurudisha nyuma shughuli zote za maendeleo zilizokuwa zikiwanufaisha wakazi wa jiji hilo na mikoa jirani
Sanjari na hayo Chalamila amesema kuwa kutokana na maelelezo ya Rais Serikali mkoani humo imeendelea kuhakikisha jiji hilo linarejea na linarejesha huduma zake muhimu za kijamii ikiwemo huduma ya usafiri wa mwendokasi na kurejesha amani yake kama ilivyokua awali.


