Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari amelikaribisha Shirika la Yeryüzü Doktorları (Doctors Worldwide Turkey) kushirikiana na hospitali za Tanzania ili kupanua wigo wa huduma nchini ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na kambi za matibabu kwa ajili ya kuwezesha wananchi wengi kunufaika na huduma bora za afya na uwekezaji katika sekta hiyo. 

Balozi Bakari alitoa mwaliko huo wakati alipolitembela Shirika hilo lililopo Istanbul, Uturuki na na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Dkt. Ahmet Salduz Novemba 28, 2025.

Mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano kwenye sekta ya afya kwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele kwa Tanzania ili ushirikiano huo uwe na manufaa zaidi kwa wananchi na jamii kwa ujumla.

Shirika hilo tayari limeanzisha Kituo cha Afya kilichopo Wilayani Kongwa, jijini Dodoma kilichofunguliwa Julai mwaka huu na kinaendelea kutoa huduma.

Balozi Bakari alllishukuru Shirika hilo lenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 kwenye sekta ya afya na kutekeleza miradi kwenye nchi zaidi ya 83 duniani kwa mchango wake katika kuimarisha huduma za afya nchini.

Tanzania na Uturuki zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya, hususan kwenye maeneo ya msingi kama vile mafunzo ya kitaalamu, kambi za afya na matibabu ya ubingwa.