Na Deodatus Balile, JamhuriMedia,Nairobi
Makala hii naiandika leo Novemba 29, 2025 nikiwa hapa jijini Nairobi, Kenya. Naandika makala hii, kwanza kuwasihi ndugu zangu Watanzania, hasa vijana, kufikiria mara mbili na kufikia uamuzi wa kutoandamana hiyo Desemba 9, 2025. Nilipofika hapa Nairobi, nimekutana na mambo mawili ambayo naomba niwashirikishe ndugu zangu Watanzania.
Sitanii, jambo la kwanza ni dereva aliyenipokea kutoka Airport kuja hotelini. Alipobaini mimi ni Mtanzania, akaniambia: “Ndugu yangu, sisi matumaini yetu makubwa ilikuwa ni kwa Tanzania. Zamani ilikuwa mnakuja Kenya kununua vitu na kwenda kuuza Tanzania, ila sasa mmetupita. Sisi hapa Kenya hatuwezi kununua kiatu, nguo au begi.
“Kwa sasa mimi na Wakenya wengi, nikitaka kuvaa kiatu kizuri au kununua shati naagiza Dar es Salaam. Hapa kwetu kodi ni kubwa ajabu. Vitu ni bei ghali sana. Kodi ziko juu sana hapa Kenya. Kwenu maisha ni mazuri. Mnajenga barabara, mna reli ya kisasa ya SGR inayotumia umeme tofauti na kwetu hapa ambapo ‘manyang’au’ walituibia wakajenga reli sub-standard inayotumia dizeli. Kwenu Mama Samia anafanya kazi kubwa na nzuri.
“Jambo moja tu, Rais Samia amechonganishwa. Ameshauriwa vibaya kumkamata Tundu Lissu na hilo ndilo Wazungu wanaonyonya nchi zetu walikuwa wanatafuta litokee. Ameingia kwenye mtego wao. Mwambie afanye kama hapa Kenya. Azungumze na Lissu kama Mtanzania, wakae pamoja, wakatae hila za Wazungu, wajenge nchi yenye utulivu… maandanano yameiharibu Kenya. Msiende njia hii si salama,” ameniambia dereva huyo.
Dereva huyu hakunifahamu hata kwa jina, ila anaonyesha kuifahamu Tanzania. Amelalamikia bei ya mafuta ya petroli na dizeli nchini hapa. Ni kweli wakati sisi hapo Tanzania lita moja ya petroli na dizeli ni wastani wa Sh 2,700 kwa bei zilizotangazwa na Ewura, hapa Kenya ni Ksh 187, ambayo kwa kubadili Sh 1 ya Tanzania na Sh 23 za Kenya lita moja ni wastani wa Sh 4,300 za Tanzania. Hapa unazungumzia wananunua lita moja ya mafuta kwa bei iliyo juu kwa zaidi ya Sh 1,300 za Tanzania. Hivi sisi lita ikiuzwa Sh 4,300 siku hiyo itakuwaje?
Sitanii, jambo la pili nililosema niwashirikishe, ni Novemba 27, 2025 hapa Kenya kulikuwapo uchaguzi mdogo katika majimbo sita. Majimbo haya ni Banisa, Malava, Kaspilu, Mbeere North, Magarini na Ugunja. Hapa Kenya wana Katiba Mpya tangu mwaka 2010. Tukumbuke mwaka 2007 walimwaga damu ya zaidi ya watu 3,000 kutokana na madai ya Katiba Mpya kuwa ikipatikana vurugu za kisiasa zingekwisha. Katiba Mpya waliipata.
Kilichotokea ni kinyume cha matarajio ya dunia. Katika uchaguzi huu mdogo, wafuasi wa vyama vya siasa wamekatana mapanga, kupigana risasi, bunduki zimeibwa na magari yamechomwa moto. Majimbo yaliyopo Mlima Meru, wanatuhumiana kuwa serikali imetumia rushwa zaidi ya Ksh milioni 700 kushinda jimbo moja la ubunge kwa ajili ya kuonyesha ina nguvu kwenye ‘Mlima’.
Vurugu na machafuko vimeshuhudiwa katika majimbo mbalimbali ambako umefanyika uchaguzi mdogo nchini hapa, huku madai ya kuwahonga wapiga kura yakishamiri katika uchaguzi kwenye maeneo hayo sita yaliyokuwa yanachagua wabunge wake.
Jimbo la Kasipul, Mbunge Peter Kaluma amejeruhiwa na wafuasi wa upinzani wa Chama cha ODM, huko Malava magari ya mgombea wa Chama cha DAP K Seth Panyako yamechomwa moto na mengine kupopolewa mawe, na ya kiongozi wa chama chake Eugine Wamalwa naye yamechomwa moto.
Katika eneo la Mbeere North wapiga kura na viongozi wa upinzani walizua vurugu kwa madai ya wapiga kura kuhongwa na watu wanaodaiwa kuwa maofisa wa serikali na wabunge.
Zaidi ya watu 30 wamelazwa hospitalini kutokana na majeraha ya panga yaliyowasibu katika uchaguzi mdogo nchini hapa. Huko Baringo walipiga kura kumchagua seneta wao, huku kata 17 zikishiriki uchaguzi wa madiwani.
Sitanii, nimegusia uchaguzi mdogo wa Kenya kuonyesha hatari iliyopo kwa nchi zetu hizi za Afrika Mashariki. Rais William Ruto hivi karibuni amekemea wanaharakati na kuitaja taasisi ya Ford Foundation ya Marekani kuwa inagawa fedha nchini Kenya kwa nia ya kuchochea vurugu za kisiasa. Taasisi hii ya Ford Foundation imethibitika kuwapa fedha zaidi ya Sh bilioni 21 wanaharakati hapo nchini Tanzania, akiwamo Maria Sarungi anayechochea Watanzania waandamane.
Kwa mwaka 2025 pekee, Maria Sarungi aliyepo hapa Kenya amepokea mikupuo miwili kutoka Ford Foundation. Mkupuo wa kwanza amepokea Sh bilioni 1.47 (1,470,000,000) na mkupuo wa pili amepokea Sh milioni 441 (441,000,000). Wapo waliopokea hadi bilioni 4, ila siwataji kwani sijaona wakifanya harakati za kusambaratisha taifa la Tanzania kama anavyofanya Sarungi, ambaye anaishi ughaibuni.
Nafahamu kuwa Sarungi amepeleka vijana wengi kwenye mafunzo nchi mbalimbali ikiwamo hapa Kenya kupitia taasisi yake ya Change Tanzania.
Wamo pia wanasheria ambao amewapa mafunzo haya, waandishi wa habari na kada mbalimbali alizoziandaa kufanya ‘mapinduzi’. Ametoa mafunzo kwa vijana katika baadhi ya vyama vya siasa na baadaye akawaelekeza cha kufanya, wakapindua wenyeviti wao. Alidhani uzoefu alioupata wa kupindua wenyeviti wa vyama vya siasa, vivyo hivyo ingekuwa rahisi ‘kuipindua’ serikali.
Sitanii, nimesema mara kadhaa na wala sioni tabu kulirudia hili. Kwamba Watanzania wanakerwa na tabia ya ‘watu wasiojulikana’ kupoteza watu. Watanzania hawapendi kuona baadhi ya watu wanapata utajiri usioelezeka. Vijana wanakereka kuhitimu chuo na sekondari wasipate kazi za kufanya. Baadhi ya polisi wamegeuka kero kwa wananchi kwa kukamata watu bila maelezo na kuwafungulia mashitaka yasiyoelezeka.
Kuna kero katika sekta ya ardhi. Rushwa iko njenje. Hospitalini baadhi ya madaktari na wauguzi hawafanyi kazi yao sawasawa. Kufanya biashara hapa nchini kwa muda mrefu imechukuliwa kama jinai, kwani ni kazi ngumu kuanzisha biashara na kuiendesha. Mambo haya ni kero kwa Watanzania na wageni mbalimbali wanaotafuta fursa za biashara nchini. Lakini kumbe ukiwa mwenyewe haujui kuwa angalau una nafuu, unaharibu hata ulichonacho. Wakenya wanatueleza hali ilivyo mbaya kwao hapa na wanaona heri wangekuwa hapo Tanzania.
Sitanii, kwa kuyatambua haya, serikali ilikubali mfumo rasmi wa kutoa sera mbadala. Mfumo huu ulikubaliwa mwaka 1992 wa kuwa na vyama vya upinzani. Vyama hivi vinapaswa kunadi sera zake kueleza wananchi iwapo vitachaguliwa vyenyewe vitafanya nini ili kuondoa kero hizi.
Hata hivyo, kuanzisha vyama pekee hakutoshi. Inapaswa kuonekana uwapo wa ushindani wa kweli katika uchaguzi bila wapinzani kuminywa au chama tawala kupendelewa. Uwanja sawa wa kufanya siasa ni jibu sahihi kabisa linalopaswa kutamalaki hapa nchini.
Wala haijaanza leo. Nchi hii ilikuwa na kodi nyingi za kero. Kwa wasiojua historia yake, hawajui zilifutikaje. Mwaka 2004/2005, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilianzisha kampeni ya kupinga kodi za manyanyaso. Nilisafiri na akina Bob Makani, Freeman Mbowe, Grace Kiwelu, Jomba Coy, Shaibu Akwilombe, Jacob Nkomola na huko Tarime wakamvuna aliyekuwa Diwani wa NCCR-Mageuzi, Rasta Chacha Wangwe.
Viongozi hawa walizunguka Kanda ya Ziwa wakieleza ubaya wa kodi ya kichwa, kodi ya baiskeli, kodi ya mifugo, kodi ya mbwa, ushuru wa minada, ushuru wa mazao… na nyingine nyingi ambazo zilikuwa zinawatia kifungoni wananchi. Mikutano ile ilimfanya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Pesambili Mramba (Mungu amlaze mahala pema peponi), katika bajeti ya Juni, 2005, alifuta kodi zote hizi.
Katika kuzifuta kodi hizi alisema: “Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Spika… naomba unielewe katika hili. Naomba kufuta kodi ya kichwa, kodi za baiskeli, maguta… maana hizi kodi kwa upepo ulivyo huko nje tunapoelekea zina madhara zaidi kuliko faida. Waheshimiwa wabunge naomba mnielewe. Napendekeza tuzifute hizi kodi (makofi).”
Sitanii, shinikizo la kisera la akina Mbowe na wenzake niliowataja lililazimu serikali kufuta kodi hizi za kero kwa nia ya chama tawala CCM kujihakikishia ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Kwa bahati mbaya sana, uchaguzi na siasa za sasa hazina tena sera. Wenyeviti wa vyama wanasimama kwenye majukwaa kulalamika na kuvurumisha matusi.
Lengo la kuanzisha vyama vingi lililokusudiwa la vyama kutoa sera mbadala limewekwa kando. Kwa sasa viongozi wa kisiasa wamejinasibu na kupambana na watoto wa wakubwa. Wamekwishaona kuwa wakiwaambia Watanzania kuwa mali fulani kama vituo vya mafuta vya Lake Oil zinamilikiwa na mtoto wa Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, Ridhiwani, itajenga chuki na kweli tumeshuhudia vituo vya mafuta vya Lake Oil vikichomwa moto Oktoba 29, 2025 kwa hoja hii ya kumilikiwa na Ridhiwani.
Badala ya kuzungumza sera mbadala kama Profesa Ibrahim Lipumba alivyozungumza sera ya elimu katika uchaguzi wa mwaka 2000 hadi nchi hii ikabadili sera ya elimu na kuleta Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES), iliyozaa shule za Kata na Mpando wa Maendeleo ya Elimu ya Chuo Kikuu. Leo hakuna tena sera. Viongozi wa upinzani wanaishia kwenye kumtuhumu Abdul, mtoto wa Rais Samia kama vile ndiyo sera za vyama vyao. Jamii inawasikiliza inapata hasira. Tunaligawa taifa.
Sitanii. Maandamano ni suala lenye mpangilio. Waandamanaji wanapaswa kueleza lini yanafanyika, yanaanzia wapi, yataishia wapi na nani anayaongoza. Kilichotokea Oktoba 29, 2025 cha kila kona watu kufumka na kuingia barabarani, hakijafikia viwango vya maandamano. Nasikitika mno kwamba baadhi ya watu; vijana na askari Polisi wamepoteza maisha. Mungu azilaze roho za marehemu mahapa pema peponi.
Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amekutana na wahariri hivi karibuni. Ameeleza kuwa Oktoba 29, 2025 waandamanaji wamechoma ofisi za serikali 756, mabasi sita ya mwendokasi, vituo 26 vya mwendokasi, wamechoma magari binafsi 1,642, wamechoma nyumba binafsi 273, vituo 159 vya Polisi wamevichoma, wamechoma vituo 672 vya mafuta na bodaboda 2,268 zimechomwa moto.

Hapo hajataja maduka, baa walizoingia na kuchukua vinywaji, watu binafsi walipopata vipigo, bidhaa za watu kama nyanya, viazi, karoti, kabeji, mifugo iliyokuwa iuzwe ikakwama njiani na mengine mengi. Wiki iliyopita niliandika nikiwanukuu waliopoteza mali wakisema Desemba 9, 2025 watawadhibiti waandamanaji huko huko barabarani, hawatapata fursa ya kupora mali zao tena.
Sitanii, inawezekana pia serikali ilikuwa haijajiandaa hiyo Oktoba 29, 2025. Kumbe sasa wanajua hizi TikTok zikihamasisha, vijana wanatenda kweli. Huenda sasa serikali imejiandaa vilivyo kukabiliana na hao waandamanaji. Bukoba wana msemo: “Kaliba kashaija, elisa empisi.” Kwa tafsiri isiyo rasmi ‘ajifanyaye shujaa bila hofu, huliwa na chui.”
Ni katika hatua hii, nawaasa vijana. Ukiacha ukweli kwamba wanaowachochea muwe mashujaa hawapo kwenye uwanja wa vita na huko waliko wanaendelea kupokea mamilioni, tugeuke nyuma. Tuangalie yaliyotokea Oktoba 29, 2025. Maisha yaliyopotea ambayo kama viongozi wa kisiasa wangetoa sera mbadala katika uchaguzi wangeweza kuingia bungeni na hatimaye Ikulu, bila kupoteza maisha ya watu.
Sitanii, ni bahati mbaya viongozi wa kisiasa wamewafungia baadhi ya Watanzania kwenye gunia lisilotoa taarifa sahihi. Wanasema nchi yetu haina kitu, kumbe si kweli. Leo Tanzania ina umeme megawati 4,031. Kenya wana megawati 2,600, Uganda 2,400, Rwanda 406 na Burundi 166. Bado tunaambiwa hatujaendelea. Tanzania ina barabara za mwendokasi, hazipo hapa Kenya, Uganda, Rwanda au Burundi. Bado hawatwambii ukweli huu.
Tanzania ina treni ya kisasa ya umeme ya SGR inayokimbia kasi ya kilomita 160 kwa saa. Hapa Kenya walijaribu, wameishia kujenga ya dizeli kutokea Nairobi kwenda Mombasa. Sisi kilomita moja ilijengwa kwa gharama ya dola milioni 4.1, ila hapa Kenya wamejenga ya dizeli kwa dola milioni 6.8 kwa kilomita moja. Kupitia REA umeme upo hadi vijiji vyote Tanzania, kwa nchi nilizozitaja, umeme upo mijini tu.
Nihitimishe na jambo moja. Zipo nyakati ukiwa nacho haujui thamani yake, kikipotea ndipo unajua. Amani, amani, amani. Nchi ya Libya walijazwa upepo wakamwondoa Kanali Gaddafi madarakani, leo ninapoandika makala hii nchi iliyokuwa inaajiri Wazungu kutoka Ulaya, leo wanaomba msaada wa mishahara kwa watumishi wa umma.
Na hawapewi, wanakopeshwa. Tunataka kwenda huko? Kama yapo makosa, tuyarekebishe kwa kutumia sera za kisiasa, lakini si kuchoma nchi kwa maandamano ambayo tukimaliza, tunaishia kushika tama. Turidhiane. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827
