Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, wameishukuru Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa RISE kwa kuanza kukarabati barabara ya Mabogini–Kahe ambayo kwa miaka mingi ilikuwa katika hali mbaya na imekuwa chanzo cha adha kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 31 imekuwa ni changamoto kwa wakazi wa Mabogini na vijiji vya jirani, hasa nyakati za mvua ambapo ilikuwa haipitiki kutokana na mashimo, maporomoko ya maji na kukosekana kwa mifereji ya kupitisha maji.
Wakizungumza, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamesema hatua ya Serikali kuanza ukarabati wa sehemu ya barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe imeanza kuleta nafuu kubwa katika usafirishaji wa mazao na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.
Bw. Hasani Halifa mkazi wa Mabogini amesema kuwa barabara hiyo licha ya kuwa bado ina changamoto katika baadhi ya maeneo, lakini imeleta unafuu wa takribani asilimia 60 kwa wakulima na wasafirishaji.
“Kabla ya ukarabati huu, tulikuwa tunasafirisha mazao kwa gharama kubwa nauli ilikuwa kati ya Sh. 7,000 hadi Sh. 10,000 kwa mzigo mmoja kutoka shamba hadi sokoni lakini sasa tunatumia Sh. 1,000 hadi Sh. 2,000 tu”, alisema.
Kwa upande wake, mkulima na kiongozi wa skimu ya umwagiliaji ya Kaloleni, Bw. Hamis Mohamed amesema kuwa awali walikuwa wakipata hasara kubwa kutokana na kushuka kwa bei ya mazao sokoni kwa sababu wanunuzi walishindwa kufika mashambani kutokana na hali mbaya ya barabara.
“Mazao yalikuwa yakiozea shambani, tulishindwa kuyatoa kwa wakati, wakati mwingine hata kupatikana kwa magari ilikuwa shida. Mradi huu wa barabara kwetu wakulima ni wa thamani kubwa” alisema.
Hata hivyo, wakazi hao wameiomba Serikali kuendeleza ukarabati huo kwa kuweka lami nyepesi ili barabara hiyo iweze kudumu zaidi na kuhimili hali ya hewa ya eneo hilo, hususan mvua kubwa na jua kali linalosababisha vumbi.
Naye, Mwenyekiti wa Kkitongoji cha Mabogini Juu, Bw. Zuberi Bakari amesema hali ya barabara hiyo ilikuwa mbaya kiasi kwamba watoto walishindwa kwenda shule msimu wa mvua huku wajawazito wakikosa huduma za afya kwa wakati, jambo lililosababisha hata baadhi yao kupoteza maisha.
“Tulikuwa tunapitia shida kubwa nyakati za mavuno, mazao mengi yalikuwa yanaharibika mashambani. Hali ya barabara ilikuwa ya kuumiza moyo. Tunaiomba serikali ituwekee hata lami ya kiwango cha kati”, alisema.
Naye, Meneja wa TARURA wilaya ya Moshi, Mhandisi Godfrey Mbema alieleza kuwa barabara ya Mabogini–Kahe ina urefu wa kilomita 31, ambapo kwa sasa kiasi cha kilomita 1.2 kimeanza kukarabatiwa kwa kiwango cha changarawe chenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 800, ikiwa ni sehemu ya mpango wa muda mfupi wa kuboresha miundombinu ya vijijini.
Serikali kupitia TARURA imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara katika maeneo ya vijijini kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi kupitia miundombinu bora inayowezesha biashara, usafirishaji na upatikanaji wa huduma za kijamii.



