Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Wadau mbalimbali wa maendeleo katika sekta ya kilimo hapa nchini wameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ‘Biodiversity for Opportunities, Livelihoods and Development’ (BOLD), unaolenga kuinua sekta ya mbegu kwenye nchi zaidi ya 50 duniani ikiwemo Tanzania, kupitia tafiti zinazoendelea kufanyika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti pembezoni mwa warsha inayoendelea ya wadau wa mnyororo wa thamani wa rasilimali za vinasaba vya mimea inayofanyika kwenye Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (World Vegetable Center) jijini hapa, wameelezea kufurahishwa na utekelezaji wa mradi huo.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utafiti wa Kilimo la Brazil, Bw. Elcio Guimaraes (katikati) akizungumza na wadau wa sekta ya mbegu wakati wa warsha ya siku tano kutathmini hali ya mradi wa Biodiversity for Opportunities, Livelihoods and Development (BOLD) ulioangazia kuinua sekta ya mbegu kwenye nchi zaidi ya 50 duniani kupitia tafiti, kushoto ni Dkt. Aloyce Kundy kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA).

Mratibu wa mradi huo kutoka Global Crop Diversity Trust (Crop Trust), Bw. Benjamin Kilian amesema mradi huo utakuwa mkombozi kwa wakulima wadogo, kwani umebeba malengo saba yatakayo leta matokeo endelevu kwenye tafiti za mbegu sambamba na kuongeza uzalishaji na uchakataji wa mazao yaliyosahaulika.

“Miongoni mwa malengo ya mradi huu ni pamoja na kuimarisha uwezo na rasilimali, kuwezesha upatikanaji wa utofauti mpya wa mbegu, kuunganisha mabenki ya mbegu , wakulima na mifumo ya mbegu, kuhifadhi nakala salama katika hifadhi ya mbegu ya dunia ya Svalbard pamoja na kuongeza uzalishaji na uchakataji wa mazao yaliyosahauliwa na yanayotumika kidogo Barani Afrika,” alieleza Bw. Kilian.

Bw. Kilian aliongeza kuwa siku tano, watashiriki pia katika vikao vya ushirikiano, mijadala ya sera, na ziara za shambani ili suluhisho za pamoja zinazoweza kutekelezeka kwa mifumo ya chakula imara na jumuishi.

Mkurugenzi Mkaazi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (World Vegetable center), Bi.Colleta Ndunguru (Wapili kushoto) akizungumza na baadhi ya wadau waliotembelea mashamba darasa kujifunza wakati wa warsha ya siku tano kutathmini hali ya mradi wa Biodiversity for Opportunities, Livelihoods and Development (BOLD) ulioangazia kuinua sekta ya mbegu kwenye nchi zaidi ya 50 duniani kupitia tafiti, Kulia ni Bw. Elcio Guimaraes mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utafiti wa Kilimo la Brazil na kushoto ni Dkt. Francis Ogbonnaya kutoka Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Nafaka

“Mradi huo unakwenda kuleta mapinduzi makubwa hususani katika kuboresha miundombinu na vifaa, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi kuhusu uendeshaji wa benki ya vinasaba, kuweka mfumo wa usimamizi wa ubora sambamba na kushirikisha makundi ya watumiaji,” alisema ba kuongeza kuwa pamoja na kuwahusisha wazalishaji wa awali, wakulima, maafisa ugani, watafiti na wadau wengine katika sekta ya mbegu.

Aidha Bw. Kilian aliipongeza Taasisi yaWorldVeg kwa kuwakutanisha pamoja wadau katika sekta ya kilimo, na kubainisha kuwa wamekuwa wakisaidia benki za kitaifa za vinasaba duniani kote, na Tanzania ni miongoni mwa washirika wao wakubwa.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Taifa cha Hifadhi ya Nasaba za Mimea kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Dkt. Mujuni Sospeter Kabululu alisema kwa upande wa Tanzania, wanashiriki katika vifurushi vitatu vya kazi kati ya vile saba, kwa kuangalia jinsi watakavyoimarisha mifumo ya mbegu, mifumo ya uhifadhi katika mazao manne ambayo ni zao ulezi, njugumawe, viazi vitamu na moringa.

“ Mazao haya yalichaguliwa kupitia kikao cha wadau tulichokaa kuchagua ni aina gani ya mazao yaingizwe kwa ajili ya kuyafanyia tafiti pamoja na kuongeza matumizi yake,” alisema Dkt. Kabululu.

Alisema kupitia mradi huo, kituo kimepiga hatua kubwa kwani wamepata vifaa vya maabara pamoja na vifaa vya kuimarisha mifumo ya uhifadhi wa taarifa za nasaba za mimea pamoja na kuongeza uhusiano wao na wadau wote wanaohusika na uhifadhi na matumizi endelevu za nasaba za mimea.

Naye Mkurugenzi Mkaazi wa WorldVeg, Bi. Colleta Ndunguru alisema wamekuwa na wasaa mzuri kwani mradi huo umeweza kuwaweka pamoja wataalamu zaidi ya 40 kujadili namna bora ya kuhifadhi nasaba za mimea pamoja na kuhifadhi mbegu za asili sambambana kubadilishana uzoefu utakaochangia kukuza sekta ya mbegu duniani.

“ Tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu na wadau wetu ambao ni Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) pamoja na Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) katika kubadilishana uzoefu na ujuzi utakao tusaidia kuzalisha mbegu zinazohimili magonjwa pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi,” alisema Bi. Ndunguru.

Naye Dkt. Adolf Saria kutoka TOSCI, alisema mradi huo utasaidia kuhakikisha mbegu ambazo zimesahaulika hususani mbegu za mazao ya mboga mboga, ambazo mara nyingi hazifanyiwi utafiti wa kutosha na vinasaba vyake havitumiki na watafiti wa ndani katika kuzalisha mbegu bora, mbegu hizo zinahifadhiwa na na kutumika kwenye tafiti, ili kuboresha aina za mbegu mpya ambazo zitamnufaisha mkulima.

“ Sisi kama TOSCI tutahakikisha mbegu zinakidhi viwango vya kitaalamu vya ubora wa mbegu, ili ziweze kusaidia wakulima kwani wanazipenda ni mbegu zao muda mrefu, ziingie kwenye utaratibu mzuri ambao zinaweza zikazalishwa kwa wingi ili nao wakulime wanufaike na mbegu hizo,” alisema Dkt Saria.

Mradi huo unafadhiliwa na serikali ya Norway na kutekelezwa na ‘Crop Trust’ chini ya wabia wake katika nchi zaidi ya 50 duniani.