Na Mwamvua Mwinyi, JanhuriMedia, Kibaha
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas, ametoa rai kwa wakuu wa idara na watendaji kuacha kufanya kazi kwa mazoea, na badala yake kuongeza uwajibikaji ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo.
Aidha, amewataka madiwani kuwa waadilifu na kutanguliza maslahi ya wananchi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa lengo la kuleta maendeleo ya kweli.

Dkt. Nicas alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mkutano wa kwanza wa Baraza la Madiwani, uliolenga kula kiapo, kuchagua Meya, Naibu Meya pamoja na wajumbe wa kamati za kudumu.
Alisema huu ni wakati wa watendaji na wakuu wa idara kujitathmini na kwenda sambamba na kasi ya maendeleo, ili kuhakikisha wananchi wanapata matokeo chanya na kuendelea kufurahia huduma wanazozipata.
“Wananchi wategemee kicheko. Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo, Mimi nitakuwa sauti ya wanyonge wasio na sauti, Kila Jumanne na Alhamisi nitatenga muda maalum wa kusikiliza kero za wananchi,” alisema Dkt. Nicas.
“Tumepewa dhamana ya kuwatumikia wasio na sauti. Mimi nahitaji kazi tu, sitaki rushwa,” aliongeza Nicas.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini, Mwl. Mwajuma Nyamka, aliwasihi madiwani na watendaji kuwa wamoja, kuonesha upendo na mshikamano katika utekelezaji wa majukumu yao.

Nyamka aliwataka kuacha yaliyopita, kuangalia yaliyo mbele na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na Ilani ya CCM ya 2025–2030.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon, alisema huu ni wakati wa matokeo na kuwasihi madiwani kuhakikisha wanaendelea kuleta tija na maendeleo kwa wananchi.
Katika mkutano huo, Dkt. Nicas alichaguliwa kuwa Meya wa Kibaha kwa kipindi cha miaka mitano, huku Aziza Mruma akichaguliwa kuwa Naibu Meya kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Dkt. Rogers Shemwelekwa, aliwakabidhi madiwani vishikwambi na vifaa vingine vya kazi kwa ajili ya kuanza rasmi safari ya uongozi wao.

