Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MATUMIZI makubwa ya teknolojia ya kisasa na akili mnemba yamerahisisha utoaji wa huduma za afya hususan upasuaji na kwenye kufundishia wanafunzi wanaosomea tiba.

Hayo yamesemwa leo na Makamu Mkuu wa chuo Kikuu Kairuki, Profesa Yohana Mashalla, wakati akizungumza kwenye mahafali ya chuo hicho yaliyofanyika kwenye kampasi yake ya Boko jijini Dar es Salaam.

Kwenye mahafali hayo jumla ya wahitimu 426 walitunukiwa vyeti, Shahada, Stashahada na Shahada za uzamili baada ya kufaulu mitihani yao ya mwisho chuoni.

“Kati ya wahitimu hao 426, wanawake ni 275 na wanaume ni 275 na wanaume ni 151 kwa hiyo wavulana lazima tujiulize tumekosea wapi, kwenye ustawi wa jamii tunawanawake 18 ambao watapata stashahada ya ustawi wa jamii,” alisema

Alisema teknolojia kwa sasa haiepukiki kwani hata kwenye chuo chao shughuli zote zimekuwa zikifanyika kwa njia ya teknolojia ya habari na mawasiliano TEHAMA.

Alisema teknolojia ya ufundishaji inasaidia badala ya mwalimu kuwa darasani wakati wote akatumia teknolojia na kuongea na wanafunzi popote pale alipo hali ambayo inapunguza matumizi ya muda.

Alisema matumizi ya teknolojia pia yanamsaidia mwanafunzi kutafuta vitu anavyotaka kujifunza na kwamba siri kubwa ya mafanikio ni kuwa na mtandao wa kutosha.

“Na kwa sasa sisi hapa Kairuki tuna uwezo wa Megabite 400 na tumewekewa mtandao mwingine unaotumika ulimwengu mzima ambapo mwanachama yeyote wa chuo kikuu kinachotambulika duniani anaweza akaenda mahali popote na kupata taarifa anazohitaji,” alisema

Alisema katika tiba teknolojia imekua msaada mkubwa akitoa mfano kuwa hospitali ya Kairuki ilishaachana na utaratibu wa mgonjwa kuzunguka na mafaili kwenda kwa madaktari.

Alisema teknolojia imesaidia kurahisisha mambo mengi ambapo sasa daktari anayefanya upasuaji halazimiki kutumia mikono yake badala yake anatumia roboti kuongoza shughuli nzima ya upasuaji.

Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Dk Donald Mmari alisema tangu kuanzishwa kwake Chuo cha Kairuki kimetoa mchango mkubwa sana kwa kutoa watumishi wa afya kwenye maeneo mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa wa wanawake, watoto na wa upasuaji.

Alisema pamoja na mchango mkubwa wa chuo hicho bado kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta ya afya hivyo kuna umuhimu wa vyuo kutoa wahitimu wengi.

Alisema idadi ya wananchi wanaohitajika katika kila wananchi 100,000 bado ni pungufu kulinganisha na viwango vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO)

“Nawaasa vyuo kama Kairuki na vyuo vingine ambavyo vinafundisha watumishi wa sekta ya afya kuongeza udahili ili kutoa wahitimu wengi ili wakazibe pengo lililopo kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Elimu ya Afya Kairuki (KHEN), Kokushubira Kairuki, aliishukuru serikali kwa miongozo ambayo imeendelea kukipa chuo hicho kila siku.

Alisema chuo hicho kinaendelea kukua mwaka hadi mwaka na kwamba takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa tangu chuo hicho kianze mwaka 1997 kimeshatoa wahitimu 3,718 .

“Tukijumuisha na wahitimu wa leo tutakuwa na jumla ya wahitimu 4,144 ambao kati ya hao 2,000 ni madaktari na 424 ni wauguzi, madaktari bingwa 135 tunaona wahitimu hao ni mchango mkubwa sana kwa nchi yetu,” alisema

Alisema licha ya changamoto za hapa na pale chuo hicho kimeendelea kujitahidi kutoa elimu bora kwa wahitimu kukidhi mahitaji ya kitaifa na kimataifa kwenye sekta ya matibabu.

“Nawapongeza wahitimu wote kwa kufaulu masomo yao vizuri nawasihi muendelee kuzingatia kazi zenu kwa weledi ili muwe mfano wa kuigwa kwa vizazi vijavyo mkawatumikie wananchi kwa weledi mkubwa sana,” alisema

“Jana kwenye kongamano mliona wenzenu waliosoma hapa Kairuki wanafanyakazi kwenye maeneo mbalimbali tena kwa nafasi kubwa naomba nanyinyi mkawe kama wao msituangushe,” alisema