Na Mwandishi wa OMH
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imeibuka Mshindi wa Pili – tuzo za Uandaaji Bora wa Taarifa za Fedha 2024 (Kundi la Idara za Serikali Zinazojitegemea) kutoka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA).
Tuzo hiyo ilikabidhiwa usiku wa Alhamisi, Desemba 4, 2025, jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, ikiwa ni sehemu ya kutambua taasisi zinazozingatia viwango, weledi na uwazi katika uandaaji wa taarifa za fedha za mwaka.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Fedha wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Hassan Mohamed, alisema mafanikio hayo yametokana na uandaaji mzuri wa taarifa za kihesabu kwa kufuata miongozo na kanuni.
Aidha, alisema, hilo lisingewezekana bila kujituma kwa watumishi pamoja na uongozi madhubuti wa Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu.
Ameeleza kuwa OMH, ikiwemo Kurugenzi ya Fedha na Uhasibu, imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi, kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuendelea kuwa mfano wa kuigwa katika uandaaji wa hesabu, jambo linaloongeza imani kwa Serikali, wawekezaji, mashirika na taasisi zinazosasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Ikiwa kama wasimamizi wa mashirika na taasisi za serikali tafsiri ya tuzo hii ni kuwa tunaongoza kwa mfano—tunafuata miongozo na kanuni katika uandaaji wa mahesabu,” alisema Bw. Mohamed, ambaye katika usiku huo wa tuzo aliambatana na Bi. Naomi Lucas, Mkurugenzi Msaidizi-Sehemu ya Fedha na Uhasibu.
Aidha, ushindi huo unaashiria mambo muhimu ikiwemo uthibitisho wa uwazi na uwajibikaji, uweledi katika uandaaji wa taarifa za fedha na kuongezeka kwa ufanisi wa OMH.
Tuzo hiyo pia imeelezwa kuwa ni chachu kwa timu nzima ya Fedha na uhasibu, na uongozi kuendelea kuongeza ubunifu na kuzingatia viwango vya kimataifa katika usimamizi wa rasilimali za umma.
Nafasi ya kwanza katika kundi hilo la Idara za Serikali zinazojitegemea ilienda kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).




