Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakar Kunenge, ametoa wito kwa wakulima wanaotumia maji ya Mto Ruvu kwa shughuli za kilimo kusitisha matumizi hayo kwa muda hadi mvua zitakapoanza kunyesha kwa wingi.

Wito huo umetolewa wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua na kutembelea mitambo ya uzalishaji maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu.

Kunenge amesema ,mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha kupungua kwa kiwango cha maji, hususan katika eneo la Ruvu Chini, hali inayochochewa na ongezeko la shughuli za kibinadamu kandokando ya mto huo.

Ameeleza ,uzalishaji wa maji katika Ruvu Chini umepungua, japokuwa si kwa kiwango kikubwa, huku Ruvu Juu ikiendelea kuwa na kiwango cha maji cha kuridhisha.

Amewataka wananchi kutumia maji kwa umakini na kuyabana kwa matumizi muhimu hadi msimu wa mvua utakapoanza.

Vile vile Kunenge amesema, kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upungufu wa maji, kwani bwawa hilo litaruhusu uhifadhi wa maji ya kutosha bila kutegemea mvua za msimu.